MADIWANI wa Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama, wamehoji
watoto wanaosoma na kumaliza katika shule za sekondari za kata huku
wengi wao wakiambulia kupata alama sifuri na kusababisha kubaki
vijijini bila mwelekeo wa maisha.
Hoja hiyo ilikuja katika kikao cha baraza lao la madiwani wa
halmashauri hiyo baada ya Diwani wa Chona, Mohamed Mwarabu (CHADEMA)
kuhoji mpango wa kuwanusuru vijana hao ambao wengi wamejiingiza katika
usanii wa nyimbo zisizokuwa na tija.
Mwarabu alisema sifuri kwa wanafunzi hao ni ukosefu wa walimu kwenye
shule hizo na hata wale wenye masomo ya Kilimo, Kiswahili na
Kiingereza hawapo, hali inayofanya wanafunzi hao wamalize elimu ya
sekondari sawa na wale waliomaliza darasa la saba.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu,
Isabela Chilumba, alidai wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kupata
alama sifuri hawako sawa na waliomaliza darasa la saba.
Chilumba alisema faida ya mwanafunzi aliyesoma sekondari ni nyingi,
ambazo si kufaulu peke yake na kuwa hata kuanza maisha atakuwa na umri
mkubwa kuliko yule wa darasa la saba ambaye huanza kupambana na maisha
akiwa na umri mdogo.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Tabu Katoto, aliwataka
madiwani hao suala la ukosefu wa walimu lisiwakatishe tamaa ya
kusimamia ujenzi wa sekondari nyingine, kwani suala hilo litamalizika,
kwa kuwa kila mwaka serikali inaajiri walimu.
Katoto alisema halmashauri yake inatarajia kufungua sekondari tatu
katika mwaka huu wa fedha, mwaka 2014/2015 katika kata za Igunda,
Nyankende na Sabasabini.
Chanzo;Tanzania Daimaa
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment