Home » » Tanesco Shinyanga yapiga dana dana walioghushi vyeti

Tanesco Shinyanga yapiga dana dana walioghushi vyeti

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
 
Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mkoani Shinyanga, linapiga danadana kuwachukulia hatua za kisheria wafanyakazi 16 wanaotuhumiwa  kughushi vyeti na kujipatia ajira kwa njia za udanganyifu.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga (RPC), Januari 24, mwaka huu, aliliandikia barua shirika hilo yenye kumbukumbu SHR/A.2/7/VOL1/279 kulishauri liende Polisi Wilaya Shinyanga kufungua jalada iIi hatua za kisheria zichukuliwe kutokana na makosa ya kughushi vyeti, lakini utekelezaji wake bado unasuasua.

Hatua ya RPC Shinyanga kutoa maelekezo hayo ni kutokana na shirika hilo Januari 21, mwaka huu katika barua yao ya kumbukumbu SHY/RM/STAFF/41 kuomba ufafanuzi wa hatua za kuchukua kwa watuhumiwa hao walioajiriwa kwa nyakati tofauti katika vituo vya Shinyanga, Bariadi, Kahama na Maswa.

Miongoni mwa watuhumiwa hao walioajiriwa kama wahasibu wasaidizi, msimamizi wa uhasibu, madereva na wajenzi.
Meneja wa Tanesco Shinyanga, Maugirra Gamba, akizungumzia hatua zilizofikiwa katika kuwashughulikia watuhumiwa hao alisema kuwa walibainika baada ya kufanya mawasiliano na mamlaka zinazotoa vyeti na kufanya uhakiki.

“Taratibu zinachukuliwa kuwashughulikia kwa mujibu wa taratibu za ajira ikiwamo kuwasimamisha kazi na wale wanaobainika kufanya makosa taratibu za kisheria zinafuatwa,” alisema.

Hata hivyo, hakuwa tayari kueleza lini watachukua hatua hizo licha ya kushauriwa na RPC Shinyanga.

Naye Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Joyce Ngahyoma, alipoulizwa kwa njia ya simu hatua walizochukua, alisema kuwa hawezi kutoa taarifa za ndani za shirika zinazomhusu mfanyakazi.

“Aulizwe Meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga au Meneja wa Rasilimali Watu Makao Makuu Tanesco atakuwa na maelezo zaidi,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa