MTOTO
wa miaka 12 anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Majengo
wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, (jina tunalo) amenusurika kifo baada
ya baba yake mzazi kujaribu kumchinja kwa madai ya kuchoshwa na gharama
za kumtibu maradhi yanayomsumbua.
Tukio hilo limetokea juzi saa 11
alfajiri katika Kijiji cha Majengo wilayani Kahama, ambapo mkazi wa
kijiji hicho (jina linahifadhiwa) mwenye miaka 37 alimkamata mtoto huyo
na kumchinja kwa kisu shingoni kwa lengo la kutaka kumuua.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema kusudio hilo halikuweza kufanikiwa, ingawa mtoto
huyo alipata majeraha sehemu ya koromeo. Mtoto huyo aliokotwa na
wasamaria wema alikotupwa na baba yake akiamini ameshatimiza azma yake
ya kuua.
Baada ya hapo baba yake huyo akiwa anaamini tayari ameua alijipeleka mwenyewe polisi kwa lengo la kujisalimisha.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali Wilaya ya Kahama, Dkt. Joseph Fwoma,
alithibitisha kufikishwa kwa mtoto huyo katika hospitali hiyo na
wasamaria wema waliomuokota, huku akiwa anavuja damu nyingi shingoni
kutokana na jaribio hilo la kuchinjwa.
Dkt. Fwoma alisema baada ya
kufikishwa hospitalini hapo madaktari walimfanyia upasuaji wa haraka na
kumshona sehemu ya koromeo iliyokuwa na jeraha kubwa, kisha kuongezewa
damu.
Alisema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri. Kwa upande wake
mama mzazi wa mtoto huyo ambaye walishatengana na mumewe kwa kipindi
kirefu, (jina tunalo) alisema alishtushwa na taarifa za kuchinjwa kwa
mtoto wake ambaye alikuwa akiishi naye kwa kipindi kirefu kabla ya
kuchukuliwa na baba yake siku moja kabla ya tukio hilo.
“Leo asubuhi
(jana) nimepigiwa simu na kuelezwa taarifa za kuchinjwa kwa mwanangu,
nilishtuka sana, sikuamini kwamba juzi alimchukua kwa ajili ya kwenda
kumuua, mara nyingi huwa akimchukua kwa lengo la kumtafutia matibabu,"
alisema na kuongeza;
“Kila alipokuwa akimchukua alikuwa akimrudisha,
katika siku za hivi karibuni alikuwa akilalamika mara kwa mara akidai
amechoshwa na gharama za kumtibu."
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Shinyanga, Evarist Mangalla, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hata
hivyo alisema inahisiwa baba wa mtoto huyo anasumbuliwa na matatizo ya
akili.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment