Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga kimeshitushwa na
taarifa za kuibuka kwa kundi la waganga wa jadi maarufu kwa jina la
‘Lambalamba’ au ‘Kamchape’ wanaopita vijijini wakiwachangisha wananchi
fedha kwa nguvu wakidai ni malipo ya kazi ya kuwafichua wachawi katika
maeneo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema kuzuka kwa
kundi hilo kunaweza kusababisha kuendelea kwa matukio ya mauaji ya
kikatili dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism),
kutokana na imani za kishirikina.
Mgeja, alisema ni muhimu kwa viongozi wa serikali mkoani hapa
kuhakikisha wanawasaka na kuwakamata wafuasi wa kundi hilo, ambalo
tayari limesababisha matatizo kwa wakazi wa Shinyanga vijijini huku
baadhi yao wakinyang’anywa kwa nguvu mifugo na fedha zao na kwamba,
serikali ya CCM haipaswi kufumbia macho vitendo hivyo.
"Ni lazima watendaji wetu ndani ya serikali muhakikishe mkoa wetu
unaondokana na aibu hii, mauaji haya ya kikatili yanachangia kwa kiasi
kikubwa kupoteza sifa ya mkoa…kundi hili lazima litokomezwe kwa
wahusika wote kukamatwa na kufikishwa katika vyombo ya dola, wananchi
sote tushirikiane kuwafichua, tuchukie, tulaani na tukomeshe aibu hii
Shinyanga," alieleza Mgeja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga,
Annarose Nyamubi wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya mwenyekiti
huyo wa CCM kukagua utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho,
kundi hilo linadaiwa kuingia hivi karibuni Shinyanga vijijini
likiwalazimisha wanavijiji kutoa fedha ili wafichuliwe wachawi na watu
wanaofuga ‘misukule.’
Akifafanua, mkuu huyo wa wilaya alisema watu hao wanawalazimisha
wanavijiji kila kaya itoe sh 5,000 kama gharama za kazi ya kuwasaka
wachawi katika vijiji vyao pamoja na kuwarejesha watu waliogeuzwa na
wachawi hao kuwa misukule, hali ambayo imesababisha mtafaruku mkubwa
miongoni mwa wananchi.
Nyamubi, alisema tayari lambalamba wanne wamekamatwa (majina
yamehifadhiwa), wakiwa na majina ya kaya 299 ambazo zilitakiwa kulipa
fedha hizo na katika mahojiano ya awali walisema walipewa vibali na
mtumishi mmoja wa manispaa ambaye pia ameagiza akamatwe na kuwekwa
ndani.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment