Home » » WANAKIJIJI HONGWA WALIA NA MWENYEKITI WAO

WANAKIJIJI HONGWA WALIA NA MWENYEKITI WAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANANCHI wa Kijiji cha Hongwa Kata ya Kinamapula Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, wamemlalamikia Mwenyekiti wao kwa ufisadi aliofanya katika miradi ya maendeleo ikiwemo kuuza ng’ombe wa kijiji hicho.
Walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara mbele ya Diwani wa Kinamapula, Emmanuel Ndinhwa, ambako walisema Mwenyekiti huyo anatumia madaraka yake vibaya kwa kuhujumu mali za kijiji.
Mmoja wa wanakijiji hao, Bundala Golobana, alisema kijiji kilikuwa kinamiliki ng’ombe sita ambao walitarajiwa kuja kusaidia ujenzi wa Zahanati, lakini Mwenyekiti huyo aliwauza kwa maslahi yake binafsi.
“Ameuza ng’ombe zetu kwa madai ya kukarabati ofisi ya kijiji yenye vyumba vitatu, huku tayari kukiwa na vifaa vya ujenzi kama saruji na chokaa, mbali na hivyo amekuwa hatushirikishi katika kutusomea mapato na matumizi,” alisema Golobana.
Kwa upande wake, Diwani Ndinhwa, alisema alipata muhtasari wa makubaliano ya kijiji hicho kulipwa ng’ombe sita na waliohujumu mawe kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, hivyo anashangaa kusikia ng’ombe wanne wameuzwa pasipo kushirikisha wanakijiji.
Diwani huyo, alimuagiza Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Maziku Madata, kuitisha kikao cha dharura cha Serikali ya Kijiji hicho ili kupatiwa ufafanuzi juu ya upotevu wa ng’ombe hao sambamba na ufisadi uliotumika katika kukarabati ofisi za Kijiji.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa