Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mtu mzima anapoambiwa kuwa na mambo yakitoto, anaweza kupasuka. Siyo kama mtoto ni mjinga saaaaaana, hapana. Ila mtoto huwaza kidogo, kufurahi sana na kupumzika zaidi. Mtu mwenye tabia kama hizi huwa na amani sana, watoto ni malaika wasiojua mabaya. Lipo neno lisemwalo: “Waacheni watoto waje kwangu, kwa maana Ufalme wa mbinguni ni wao.” Lakini siyo Bongo. Hapa mtu mzima anayeishi kama mtoto huwa shakani.
Ili mtu awe mtu, hana budi kuyajua maisha yake. Hana budi kuumia moyoni, kukasirika, kuwa na wivu na kadhalika. Lakini kubwa zaidi, hana budi kujua kudhibiti changamoto zote zinazomkabili, zikiwemo hizo hapo juu. Panapo na jibu ni lazima palikuwa na swali. Hivyo, ajue kuongea pale anapotakiwa kufanya hivyo na kunyamaza pale anapopaswa kunyamaa.
Yupo ambaye mambo yote hayo kwake ni misamiati. Siyo kwamba alikosa kwenda shule, lakini hakujua shule ni mdudu gani. Hakujua analala na kuamka wapi, saa ngapi, kula wapi, kula nini na saa ngapi.
Hakucheza mtaani ‘kombolela’, ‘kula mbakishie baba’, wala ‘tobo ngumi’. Huyu hata aende vyuo na kurudi na kontena la shahada, bado huwa ni shida kwenye jamii.
Tabia za utoto huakisiwa ukubwani. Unaweza kumtambua mtu mzima aliyekosa ngazi ya utoto kwa kushobokea mambo yasiyo na maana maishani.
Kwa mfano; mwanandoa anayepata kila anachohitaji, akichepuka na mfanyakazi wake wa ndani. Au bosi anayelazimisha michepuko na katibu muhtasi. Utaona kuwa watoto ni lazima wagombane na husahau muda uleule. Hivyo, ukimwona mtu mzima anatengeneza bifu, ujue ipo ngazi aliiruka bila kuiona.
Katika hili, tulimhurumia sana Michael Jackson. Kwa sababu alikuwa supastaa tokea utotoni. Alifuatwa na mapromota wakubwa, akapandishwa helikopta kwenda kufanya shoo mbali na nyumbani. Alikaa kwenye hoteli kubwa kama Hilton’s, kula kwenye migahawa mikubwa ya Macdonald’s, kutinga mavazi ghali zaidi duniani na kukutana na watu mashuhuri tena kwa kubembelezwa.
Kwa hali hiyo, aliikosa ngazi muhimu ya kuingia ukubwani. Uzeeni mwake akajikuta akijikoboa ngozi na pua, kuchezea midoli na kulala kitanda kimoja na watoto. Ghafla akapewa kesi ambayo ilimwacha kuwa masikini na akachanganyikiwa si haba. Wafuatiliaji wa mambo waliujua huo kuwa mwanzo wa mwisho wa Mfalme wa Pop aliyevikonga vizazi vitatu vya dunia.
Watu wanaokosa ngazi hukosa heshima (kwa sababu hawajui maana yake), hukosa uadilifu kwa sababu hiyo hiyo, lakini pia hukosa utu. Mimi nafahamu wazi kuwa “No research, no right to speak” (kama hujachunguza basi hauna haki ya kusema). Lakini nikishaupiga mtonji wangu, mimi nitajisemea mwenyewe, lakini siyo dhambi kwa mwenye sikio kusikia. Maneno ya usiku husikiwa hata na panya.
Mchana mmoja karibu majuma mawili yaliyopita tuliona gari iliyokuwa ikitangaza mgawo wa umeme. Tuliambiwa utatukumba kwa masaa kumi kila siku kuanzia asubuhi. Lengo la mgawo huu ni jema; ni kuondoa tatizo la muda mrefu nchini; ambapo nguzo iliyooza huweza kuanguka na kuleta kizaazaa kitaani. Tukasema Insha-Allah, Mungu alitie wepesi jambo hilo.
Kesho yake (yaani ni baada ya mchana ule, jioni na usiku wake) umeme ulikatika mapema sana. Tukajua hakuna taabu; tukahesabu masaa hadi saa mbili usiku. Umeme ukarudi kwa dakika tatu na kukatika tena. Dakika tano baadaye ukarudi na kukatika muda huohuo! Hali hiyo ilijirudia kama mara tano hivi. Siku iliyofuata hali ikawa ni afadhali ya jana. Ya tatu yake hivyohivyo.
Anyway, leo sisemi kwa kuwa sijakula mtonji. Lakini ningependa kuuliza: Ni kwa nini kwenye kitengo cha ukataji umeme yupo mtu makini na kitengo cha kuurudisha hayupo mtu makini?
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment