Home » » WANANCHI KISHAPU WAWALIZA BAWACHA

WANANCHI KISHAPU WAWALIZA BAWACHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wananchi Kishapu wawaliza BAWACHA
WANAKIJIJI wa Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wamewatoa machozi viongozi waliokuwa wameambatana na msafara wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema, (BAWACHA), Halima Mdee, baada ya kuwaonyesha majeraha ya risasi walizopigwa na polisi kwenye mgodi wa almasi Mwadui unaoendeshwa na kampuni Williamsons Diamond Ltd.
Aidha, wananchi hao walionyesha majeraha ya risasi kwenye maeneo mbalimbali ya miili, ambayo yamewasababishia ulemavu wa kudumu, ambako mmoja alionyesha mguu aliokatwa huku mwingine akionyesha jicho alilotobolewa.
Tukio hilo lilitokea juzi kwenye viwanja vya Gulio Maganzo, ambako mara baada ya Mdee kufika na msafara wake eneo hilo kwa lengo la kufanya mkutano wa hadhara, ndipo wananchi hao waliomba chama hicho kiwasaidie kupata haki zao.
Wananchi hao, walisema kuwa walikutwa na madhila hayo kwa nyakati tofauti wakati walipoingia kwenye eneo linalotumiwa kumwaga mchanga ambao tayari umeshamaliza kazi ndani ya mgodi huo, ambao wao huuchekecha kwa lengo la kubahatisha almasi iliyobaki.
BAVICHA wajitosa kuwasaidia
Akizungumza na wananchi hao, Mratibu wa Taifa wa Baraza la Vijana Chadema, (BAVICHA), Edward Simbeye, aliwapa pole wananchi hao huku akiwahakikishia kuwa atawasaidia kuwapa mwanasheria ili kuhakikisha hakuna haki ya mwananchi hata mmoja inapotea.
Mdee anena
Mwenyekiti wa BAWACHA, Mdee, alisema inasikitisha kuona wananchi wakiumizwa na kuuawa na polisi ambao jukumu lao la msingi ni kulinda raia na mali zao.
Alisema kuwa inasikitisha kuona wananchi hao wanageuzwa wakimbizi kwenye maeneo yao, wakipigwa risasi bila huruma, jambo aliloitaka Serikali kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa mara moja.
Wananchi waeleza kwa kina
Mmoja wa wananchi hao, George Bwisige, alisema kuwa alikatwa mguu wake wa kulia baada ya Septemba 1 mwaka jana kukamatwa akichekecha mchanga huo, ambako alijaribu kukimbia lakini polisi walimkamata na kuamua kumpiga risasi kwenye mguu huo.
“Tulikuwa na wenzangu watano tukichekecha mchanga, ghafla walitokea polisi nane na walinzi 10 wa kampuni, wengine walifanikiwa kutoroka tukabaki mimi na Amour Said ambaye yeye alikamatwa kabla yangu, yeye alipigwa risasi akiwa mbali kidogo akaanguka lakini waliponiona mimi wakamruhusu aondoke…
“Walinichukua wakanipiga risasi hapa (huku akionesha mguu wake wa kulia ambao sasa ameweka wa bandia), kwa karibu kabisa, wakawa wanataka kunidumbukiza kwenye shimo ili kupoteza ushahidi ndio Amour akarudi akipiga kelele, kwani hakuwa ameenda mbali kama walivyodhani. Aliwaambia ni bora wakatuua wote, ilisaidia kwa kweli walituacha,” alisema Mwisige.
Alisema kuwa baada ya hapo, polisi walimchukua na kumpeleka kwenye zahanati iliyopo ndani ya mgodi huo, ambako huko alikuwa hapatiwi matibabu ya aina yoyote hali iliyomsababishia kuoza mguu huo ambao ulianza kutoa wadudu aina ya funza.
“Nilikaa pale siku tisa bila matibabu na ndugu zangu wakitaka kunichukua walikuwa wanakataliwa, mpaka waliamua kufanya maandamano ndiyo nikaruhusiwa Septemba 19 mwaka jana, nikapelekwa hospitali ya rufaa ya Bugando Mwanza, ambapo waliuangalia mguu kitaalamu na kwa hali ilivyokuwa, kesho yake waliamua kuukata kwani ulikuwa na hali mbaya sana,” alisema Bwigise kwa masikitiko.
Alisema kuwa baada ya matibabu amekuwa akifuatilia suala hilo polisi ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, lakini amekuwa akigonga mwamba hivyo kuomba viongozi wa Chadema wamsaidie.
Alisema kuwa ugumu wa maisha ndiyo huwasukuma kwenda kwenye eneo hilo kujitafutia riziki, ambako kwa kufanya shughuli hiyo aliweza kununua pikipiki mbili lakini kwa sasa ameziuza ili kugharamia matibabu.
Mwanakijiji mwingine, Nyalu Sita, alionyesha maeneo yenye alama alizopigwa risasi na polisi ikiwemo mgongoni na mikononi, ambako rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Ben Mao, alifariki dunia kwenye tukio hilo baada ya kuigwa risasi.
Mwanakjiji Felix Mallya, alisema kuwa Februari 20 mwaka huu, alikamatwa akichekecha mchanga akapigwa risasi kwenye miguu wa kulia zaidi, hali iliyoufanya ushindwe kunyooka mpaka sasa.
Mwananchi mwingine, Jeuna Mathias, alionyesha jicho lake la kulia alilodai kuwa lilitobolewa na askari polisi wakati waliomkamata akichekecha mchanga ili aambulie walau mabaki ya almasi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majimaji, Seba Ndekelwa, (CCM), akizungumza na Tanzania daima, alikiri kutokea kwa matukio hayo huku akitupia lawama vyombo vya usalama kwa kushindwa kuwasaidia wananchi kupata haki zao.
Alisema kuwa wananchi wengi wamepigwa risasi na kufa na wengine kupata ulemavu wa kudumu, ambao alisema kwa mwaka jana pekee waliuawa vijana watatu huku mwaka huu wakiuawa wengine wanne.
Meneja Uhusiano wa mgodi huo, Joseph Kahasa, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, alikataa kutoa ufafanuzi wowote juu ya suala hilo kwa madai kuwa hana uhakika kama anayeongea naye ni mwandishi wa habari, hivyo akataka mwandishi apange siku ya kufika mgodini hapo ili akampe ufafanuzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Jostusi Kamugisha, alisema kuwa ana taarifa ya tukio moja la askari wa mgodi kumpiga mwananchi risasi, lakini hayo mengine hana taarifa nayo, hivyo akawataka hao wanaolalamika kufika ofisini kwake.
“Hizi habari ndiyo nazisikia kutoka kwako, hakuna polisi aliyepiga mtu risasi, ila mimi nina taarifa ya tukio moja la mlinzi wa mgodi kumpiga mwanakijiji risasi. Hao wanakijiji wanaokuja kwako wewe mwandishi utawasaidia nini? Waambie waje ofisini kwangu,” alisema Kamanda huyo.
Kasulumbai aibua mapya
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Mashariki, Silvester Kasulumbai, (Chadema), alisema kuwa mgodi huo ulirejeshwa serikalini tokea mwaka 1945.
Alisema kuwa kwa sasa hakuna kampuni inayoendesha shughuli kihalali kwenye eneo hilo, kwani serikali haikuwahi kutoa eneo hilo lenye ekari 18,000 kwa kampuni yoyote.
Makamu BAWACHA asisitiza mshikamano UKAWA
Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA, Hawa Mwaifunga, amewataka viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi, (UKAWA), kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Kitaifa ili kazi ya kuing’oa CCM mwakani iwe rahisi.
Alisema kuwa ni vema viongozi hao wakaweka maslahi ya Taifa mbele na kuhakikisha wanapitisha viongozi wenye sifa kugombea kwenye chaguzi mbalimbali, kuanzia za vitongoji, vijiji na mitaa zinazotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu, ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.
Mwaifunga, alisema kuwa hatua hiyo itauhakikishia umoja huo ushindi mkubwa mwakani kwenye uchaguzi mkuu na endapo watafanikiwa kuingia Ikulu, basi wananchi watarajie marudio ya mchakato wa katiba ambao utazingatia maoni na matakwa ya wananchi.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa