Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga imetajwa
kuongoza kwa kuuza pamba chafu iliyowekwa mchanga inayofikia tani 10,
kitendo kinachoelezwa kufanywa na baadhi ya watu wasio waadilifu.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Chama Kikuu cha
Ushirika Mkoa wa Shinyanga (Shirecu) juzi, Mwenyekiti wa chama hicho,
Robert Jongela aliwataka wana ushirika kujiepusha na udanganyifu akisema
unaathiri mapato na sifa ya ushirika kwa wanunuzi wa nje kuharibu
mitambo.
Jongela alisema kuwa kitendo hicho kinaweza
kuharibu sifa ya ushirika huo kimataifa kutokana na watu wachache wasio
waadilifu, huku akibainisha kuwa kwa kipindi kirefu walikuwa hawajapata
tatizo la kuuza pamba chafu.
“Hili tatizo limeibuka msimu huu wa mwaka 2014/15,
baadhi ya vyama vimeuza pamba chafu iliyowekwa mchanga kwa makusudi.
Tatizo hili limeikumba Wilaya ya Kishapu ambayo ndiyo inaongoza, mchanga
kwenye pamba uliokutwa unafikia tani 10. Ni hatari, lazima tukemee hali
hii,” alisema Jongela.
Mwenyekiti huyo alitoa onyo kwa viongozi wa vyama
vya ushirika vya msingi na watendaji wao kuwa, wasipozuia hali hiyo
inayoonyesha kuota mizizi watachukuliwa hatua kwani mkopo wanaopata
benki unatozwa riba kubwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi
alisema kuwa Serikali itaendelea kusimamia ushirika kuhakikisha
hauvunjwi wala kuingiliwa na mtu yeyote akieleza kuwa vyama vingi
vimekufa kwa kukosa usimamizi imara.
Nyamubi aliutaka ushirika huo kuanzisha kilimo cha
biashara za mazao mengine, ikiwamo alizeti ili kujikwamua zaidi
kiuchumi badala ya kutegemea zao moja kwani hivi sasa kumekuwa na
uhitaji mkubwa wa alizeti kwenye viwanda vya Wachina vilivyojengwa
Shinyanga.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment