KATIKA
hali isiyo ya kawaida, wakazi wa Kata ya Masekelo, Manispaa ya
Shinyanga, juzi walilazimika kususia mazishi ya mkazi wa kata hiyo baada
ya ndugu zake kushinikiza marehemu azikwe kwa taratibu za kimila.
Taratibu hizo ni kupasua tumbo la mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa hali ambayo iliwafanya baadhi ya wananchi wasusie mazishi hayo na kuondoka makaburini ili kuwapisha ndugu hao watekeleze matakwa ya mila yao ya Kikurya.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema marehemu (jina tunalihifadhi) ambaye ni mwanamke, alikuwa akiishi Mtaa wa Mapinduzi na siku moja kabla ya mazishi hayo, baadhi ya ndugu zake walitishia kutomzika ndugu yao kutokana na mumewe kutomlipia mahali.
Ndugu hao walishinikiza mume wa marehemu alipe sh. milioni moja kama mahari ili waweze kushiriki mazishi.
Walisema marehemu alifariki Januari mosi mwaka huu katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga wakati akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa kwa ugonjwa wa tumbo na mazishi yake kufanyika juzi mchana katika makaburi yaliyopo Kata ya Masekelo.
"Ndugu wa marehemu aliyetoka mkoani Mara, ndiye aliyeshinikiza mazishi ya ndugu yao yazingatie taratibu za mila ya Kikurya ili kuondoa mikosi ndani ya familia kutokana na ndugu wengi kufariki na ugonjwa uliokuwa ukimsumbua marehemu.
"Baadhi ya watu waliohudhuria mazishi hayo, walipinga vikali kitendo hicho na kushauri kama pangekuwa na ulazima wa kutekeleza mila hiyo, ingefanyika hospitali eneo ambalo ni faragha si kuifanya mbele ya kadamnasi ya watu," walisema.
Shuhuda mwingine alisema mgogoro huo ulianzia nyumbani kwa marehemu kabla ya kwenda makaburini ambapo baadhi ya ndugu pamoja na kuielewa hali hiyo, walionesha utulivu lakini baada ya kufika makaburini na kuanza shughuli za mazishi mmoja wa ndugu hao aliingia makaburini na wembe.
"Wakati tukiwa nyumbani, dalili za kutokea vurugu zilianza kuonekana lakini sehemu kubwa ya wanandugu walitulia hadi tulipofika makaburini na kuanza shughuli za mazishi, ghafla ndugu mmoja aliingia kaburini akiwa ameshika wembe na mikononi alikuwa amevaa mpira laini.
"Alipoingia kaburini alikuwa ameshika boksi dogo ndani yake kukiwa na kifaranga cha kuku... aliwataka wananchi waache kutupa udongo, alifungua jeneza la marehemu na kumchana tumbo lake kwa wembe hali ambayo iliwashtua watu wengi na kuamua kuondoka makaburini," alisema.
Alisema ndugu huyo alimchinja kifaranga cha kuku, damu yake kuimwagia kwenye mwili wa marehemu na kumwingiza kifaranga huyo katika tumbo la marehemu kwa lengo la kumaliza mkosi ndani ya ukoo wao.
Aliongeza kuwa, baada ya kumaliza kumwingiza kifaranga katika tumbo la marehemu, alifunika jeneza, kutoka nje na kuwaomba wananchi waliobaki waendelee kufukia kaburi.
Akielezea tukio hilo, Ofisa Mtendaji Kata ya Ndala, Bw. Dickson Venance, alisema siku moja kabla ya mazishi hayo palitokea mgogoro uliohusisha suala la mahari wengine wakitaka kuondoka na mwili kwenda kuuzika Mara.
"Nilijitahidi kuusuluhisha mgogoro huo, ndugu walikubali kulipwa sh. 100,000, upande wa mume wa ma r e h emu walichangishana na kupata fedha hizo nikazikabidhi kwa ndugu wa marehemu na kuridhia mazishi yafanyike Shinyanga," alisema Venance.
Hata hivyo, ilielezwa baadhi ya wananchi waliamua kutoa taarifa za tukio hilo Kituo cha Polisi ambao walifika makaburini wakati wa mazishi yakiendelea na kuwakamata wanandugu wote waliohusika na uendeshaji wa shughuli kimila.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanandugu wote waliohusika walikamatwa, kuhojiwa na ilipobainika ni mambo ya kimila waliachiwa.
Chanazo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment