Yapo matatizo mengi ambayo yanazuia kasi ya maendeleo ya michezo
nchini, ila wahusika wamekuwa wakiyafumbia macho na kuona kama ni
masuala ya kawaida.
Matatizo yaliyopo katika sekta ya michezo siyo ya
kawaida na kama hatutayaondoa, basi kila mwaka hatutafanya vizuri
kimataifa na tutaendelea kuona michezo haina umuhimu katika uhai wa
Taifa letu.
Michezo ni muhimu katika uhai wa Taifa, kama
tutadharau basi tujue tutasababisha mamilioni ya Watanzania wanaotegemea
michezo kwa ajili kuendesha maisha yao kuishi maisha ya dhiki.
Matatizo yanayozuia maendeleo ya michezo nchini
yapo mengi na siwezi kuyataja yote katika uchambuzi huu ila matatizo
mengine yapo wazi kabisa.
Matatizo ambayo naweza kuyataja ni uhaba mkubwa wa
vyuo vya taaluma ya michezo na upungufu wa wataalamu wa michezo,
kutofundishwa kwa somo la elimu ya michezo shuleni na kwenye vyuo,
utunzaji na usimamizi mbaya wa viwanja vya michezo vilivyopo nchini,
uvamizi wa viwanja vya michezo kwa watoto na upungufu mkubwa wa viwanja
vyenye hadhi ya kimataifa.
Matatizo mengine ni ukosefu wa viwanda vya
kutengenezea vifaa vya michezo nchini na gharama kubwa ya vifaa hivyo
vitokavyo nchi za nje, Wizara inayohusika na michezo kurundikiwa mambo
mengi yasiyohusu michezo, ufinyu wa bajeti ya kuendeleza michezo,
wananchi kukosa desturi ya kucheza kwa ajili ya afya zao na kushindwa
kuwatumia wataalamu wachache wa michezo waliopo nchini.
Pia matatizo mengine ni utawala mbovu katika vyama
vya michezo kwani watawala hao wanashindwa kutekeleza wajibu wao wa
kuendeleza michezo, Serikali nayo haina Sera bora na mipango mizuri ya
kitaifa ya kuendesha michezo vilevile hakuna muundo na utaratibu wa
utawala mzuri wa kuendesha michezo nchini.
Hayo ni baadhi ya matatizo yanayokwamisha
maendeleo ya michezo nchini na mimi naamini kabisa bila wanasiasa au
Serikali kuisapoti michezo nchini au kampuni kujitokeza na kuwekeza
kwenye michezo na viongozi wa michezo kukubali kutekeleza wajibu wao
kikamilifu hatutaweza kuona mabadiliko kwenye michezo wala kufanya
vizuri kimataifa kwani tuna matatizo mengi.
Lazima tukubali wachezaji nyota katika mchezo
wowote huandaliwa katika mazingira yatakayomwezesha kuwa mchezaji nyota
siyo kumwandaa mwanamichezo katika mazingira ya matatizo kama tuliyonayo
hivi sasa.
Ni wazi, tunatakiwa kujua umuhimu wa michezo
nchini na kujua kuwa michezo ni kiungo muhimu, ni sekta muhimu kwa taifa
kwa hiyo tuondoe matatizo yanayozuia umuhimu wa michezo.
Michezo ni muhimu kwani hujenga na kuimarisha
afya, hujenga ushirikiano, upendo, udugu na uzalendo, hujenga taifa
lenye nidhamu, uhusiano, uelewano, mshikamano, moyo wa kishujaa na
kujihami, hukuza ukakamavu, ujasiri na kujiamini.
Pia umuhimu mwingine wa michezo ni kuwapatia
wananchi burudani, kulitambulisha na kulitangaza taifa nje ya mipaka,
kumjenga mchezaji kimwili, kiakili na kiroho na kutoa ajira pana.
Ili faida za michezo zipatikane nchini ni lazima kwanza tuwe na
Sera bora, malengo na mipango ya kuhakikisha tunaondoa matatizo ambayo
ndiyo vikwazo vya mafanikio kwenye michezo.
Naamini huu ndiyo wakati wa kulikwamua taifa letu
katika janga la kukosa maendeleo ya kimichezo kwa kutambua sekta ya
michezo ni muhimu katika uhai wa Taifa letu kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment