Salamu zangu kwenu wapenzi wa darasa huru. Ni juma jingine tena
tunakutana kufahamishana mambo yanayogusa maisha yetu ya kila siku,
lengo ikiwa ni kuelimishana, kuhabarishana na kusaidiana katika kuwekana
sawa ili maisha yasonge vyema.
Kwa wale ambao wamekumbwa na changamoto mbalimbali
za maisha zilizowalazimu kusimamisha shughuli zao za kujitafutia riziki
za kila siku, nawapa pole. Nawaombea kwa Mungu awape nafuu na warejee
katika pilikapilika za utafutaji maisha na kuingiza riziki hata kama ni
kidogo, hasa mwezi huu wa kwanza ambao kwa jinsi mambo yalivyo mengi,
unaweza kutamani ardhi ipasuke uingie.
Tuachana na hilo, turejee katika mada yetu ya leo
ambayo najua inatugusa wengi wetu kwani suala la umbea ni kama jambo la
kawaida kwa baadhi ya watu. Wao bila umbea wanaona kama kuna kitu
wamekosa. Kwao umbea ni jambo la kawaida hawaoni haya kusengenya.
Zamani nilikuwa naona kama watu wa namna hiyo
hawajastaarabika. Kifupi nilikuwa nawaona kama watu wa ajabu. Lakini
baada ya kusoma majarida mbalimbali na kugundua kuwa moja ya njia ya
kupunguza msongo wa mawazo ni umbea, nikaanza kuelewa.
Mbali na kusoma majarida hayo, mwaka jana kuna
utafiti ulifanywa ukabainisha kuwa umbea unasaidia kupunguza msongo wa
mawazo. Kutokana na hilo ni dhahiri kuwa suala la umbea ni zuri katika
maisha yetu ya kila siku. Tunawashukuru watafiti hao kwa kuwafungua watu
kama mimi niliyekuwa na mawazo hasi juu ya umbea.
Kwa mfano, unaweza ukawa umekaa na mambo mengi
yanakusumbua kichwani, mara akaja swahiba wako akakupa umbea, ukafurahi
hata ukasahau yale uliyokuwa unawaza kwa muda.
Lakini kuna mambo ambayo watu wengi tunakosea
kuhusu umbea. Unaweza kukuta mtu anamzungumzia mtu fulani kwa mwenzake
au kundi la watu, lakini nusu ya maongezi yale yanakuwa siyo ya kweli.
Mambo ya uongo ndiyo yanakuwa mengi. Yaani kama ni wewe ulikuwa
unazungumziwa halafu mtu akaja kukueleza kuwa watu fulani walikuwa
wanakuzungumzia hivi na hivi, lazima utashikwa na butwaa.
Utajiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Ni
kwa nini watu wanazungumza uongo kiasi hicho? Hata kama ni umbea basi
wazingatie na ukweli. Iweje ukweli wauache, halafu waseme uongo mtupu?
Sasa huo sijui huo tuuite umbea au uzushi.
Mbaya zaidi mambo kama hayo yanaweza kusambaa na
kumharibia mtu sifa kutokana na watu wachache wasiokuwa na busara. Mtu
anajiropokea tu mambo yasiyo ya kweli hadi unashangaa kama ametumwa au
labda umemkosea, kumbe hakuna kitu. Tena ukikutana naye, anakuchekea na
kukusalimia kwa furaha zote.
Kuna mambo wakifanya watoto wadogo unaweza kuelewa
kutokana na umri wao, lakini wakifanya watu wazima wenye akili ni jambo
la kushangaza kwa kweli. Tujaribu kuwa na staha jamani hata kama
tunateta basi tujaribu kuwa wakweli. Mbonatunaacha mambo mazuri,
tunasema mabaya tu. Tuseme yote kwa usawa tukizingatia ukweli kwani
umbea hauepukiki katika maisha yetu.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment