Home » » MBATIA AANIKA KASORO SERA YA ELIMU.

MBATIA AANIKA KASORO SERA YA ELIMU.

 

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
 
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia (pichani), amekosoa sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014, iliyozinduliwa rasmi wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete, kwamba pamoja na kutumia miaka saba kuindaa, lakini ina mapungufu makubwa na haijajibu maswali magumu ya changamoto ya elimu nchini.
 
Kadhalika, amesema sera hiyo badala ya kuleta ufumbuzi wa tatizo la elimu, imeandaliwa kisiasa kwa lengo la kuwalaghai Watanzania kwa ajili  ya uchaguzi mkuu mwaka huu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana, Mbatia alisema  sekta ya elimu nchini iko mahututi na kwamba badala ya serikali kuandaa sera ambayo ingeleta majawabu ya muda mrefu imeongeza tatizo jingine.
 
Alitaja baadhi ya udhaifu uliopo katika sera hiyo mpya kuwa ni pamoja na lugha ngumu iliyotumika ambayo haieleweki kwa urahisi,  kutokuandikwa kitaalam pamoja na makosa mbalimbali ya matumizi ya lugha.
 
Pia, Mbatia alisema haijaleta suluhisho la malumbano ya muda mrefu juu ya lugha inayofaa kufundishia na kwamba inaonyesha dhahiri serikali haina nia ya dhati ya kutatua tatizo la mfumo wa elimu unayoikabili taifa kwa kufanya mchezo wa kutoa majibu mepesi kwa mambo magumu yenye mustakabali wa taifa.
 
“Sera hii mpya ya elimu imewachanganya Watanzania, imeandikwa kwa lugha isiyoeleweka, ina makosa mengi ya matumizi ya lugha, haijaweka bayana lugha rasmi ya kufundishia, inayo matamko mawili yaliyokaa sambamba, moja wapo ni kutaja  kwamba Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu,” alisema Mbatia  na kuongeza:
 
“Matamko haya mawili yamekwepa lawama zinazotokana na malumbano ya muda mrefu kuhusu ni lugha gani hasa inafaa kufundishia, pia yamehalalisha mifumo miwili ya elimu ndani ya nchi moja. Serikali ilipaswa kutengeneza sera ambayo inazungumza kwa uhakika kuhusu suala la lugha ya kufundishia kuliko kutoa tamko la sera lisilo na msimamo wa wazi.”
 
Alipendekeza kuwa ili kuondoa tatizo la elimu linaloikabili taifa hivi sasa ni vyema iundwe Tume ya kudumu ya elimu nchini, itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine kuhakikisha ubora wa elimu na kudhibiti mambo yanayoweza kusababisha kutetereka kwa ubora huo.
 
Alisema tume hiyo itakayoundwa  iwe na mamlaka ya kuhakiki utendaji wa taasisi mbalimbali za elimu ambazo hadi sasa zimeonekana kutotimiza vyema majukumu yake,  kama ambavyo ilifanyika kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Julius  Kambarage Nyerere.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa