Home » » Wagombea wanawake wawalaumu wanaume.

Wagombea wanawake wawalaumu wanaume.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
  Wadai kunyanyaswa, kutukanwa bila ya aibu majukwaani
Chama cha ACT- Wazalendo.
Wagombea wanawake wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, wamewalaumu wagombea wanaume wanaoshindana nao katika nafasi hizo, kutokana na kutumia vibaya majukwaa kwa kuporomosha matusi na kuwadhalilisha mbele ya jamii.
 
Wagombea hao wanawake kutoka mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu walipaza sauti zao juzi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kujiamini majukwaani pamoja na kufahamu namna ya kutoa sera za kukubalika kwa wananchi, yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ambayo pia yalihusisha vijana na walemavu.
 
Mgombea udiwani kata ya Chamaguha, Manispaa ya Shinyanga kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Siri Yasini na Mikwise Mahela wa nafasi hiyo kata ya Nyashimo wilaya ya Busega kupitia CCM, walisema wagombea wanaume wamekuwa wakiwanyanyasa bila ya aibu majukwaani.
 
“Siasa za matusi zimepitwa na wakati, wananchi hivi sasa wanataka waelezwe ni jinsi gani utawaletea maendeleo na kutatua kero zao na siyo unashindana na mwanamke unatumia mwanya huo kuanza kumshambulia kwa matusi ya udhalilishaji,” alisema Yasini.
 
Naye mgombea udiwani kijana katika kata ya Majengo wilayani Kahama, Jackson Daudi kupitia Chadema, alisema mafunzo waliyopewa na TGNP yamewajengea uwezo wa kujiamini pamoja na kuzifahamu mbinu za kuendesha kampeni licha ya kubaki muda mfupi kabla ya uchaguzi.
 
Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka TGNP, Happines Maruchu, alisema mtandao huo wa kinjisia umekuwa ukitoa mafunzo ya kuwawezesha vijana, wanawake na makundi maalumu ambao wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa