Home » » TASAF YAOMBWA KUTAMBUA UPYA KAYA MASIKINI.

TASAF YAOMBWA KUTAMBUA UPYA KAYA MASIKINI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Kahama wameutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kurudia kuzitambua kaya masikini katika kata mbalimbali, kwani baadhi ya watu waliopewa msaada, hawakustahili.

Hayo yalisemwa juzi na Diwani wa Malunga, Shaban Selle katika kikao maalumu kwa ajili ya kupitisha makadirio ya bajeti ya halmashuri hiyo kwa kipindi cha mwaka 2016/2017.
Selle alisema kuwa uongozi wa Mradi wa Tasaf Awamu ya Tatu (Tasaf I11), haukuwafikia walengwa katika hatua ya kuwatambua kaya masikini na kusababisha wasio walengwa kupatiwa ruzuku hizo.

Alisema kuwa kutokana na makosa hayo, ni bora ufanyike upembuzi upya kwa ajili ya kuwapata walengwa halisi ili kupunguza manung’uniko kwa wananchi.
“Pia unapowaomba viongozi wa kata wakupe orodha ya watu masikini ambao tayari wameshasaidiwa na mfuko wamekuwa wakikatalia hali ambayo imezua hofu kubwa kwa wananchi,” alisema Selle.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Abel Shija, alisema uchunguzi ufanyike ili kuondoa masikitiko kwa kaya zisizojiweza na ambazo hazijanufaika na Tasaf III awamu hii.
Shija alisema kumekuwa na udhaifu kwa baadhi ya watu kugawa fedha kwa wasiostahili.
“Kuna wengine wamekuwa wakitoka kata moja kwenda nyingine kupata msaada, huku wakisingizia kuwa wao ni waathirika wa ugonjwa hatari wa Ukimwi, jambo ambalo si sawa,” alisema Shija.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba, alisema ni kweli mfuko huo umekuwa na mapungufu.
Aliongeza kuwa hatua ya kutambua kaya masikini, inasimamiwa na kamati za vijiji na kata katika maeneo yanayohitaji msaada.
“Lazima zinufaike kaya masikini kwani zile fedha ni za serikali na zimetolewa kwa ajili ya wananchi kama hao, ambao hawajiwezi kwa mujibu taratibu za Serikali zinavyoonesha,” alisema Msumba.

Alisema kwa mara ya kwanza, waligundua kuwa kaya zilizoandikishwa hazikustahili na viongozi wa Tasaf walirudia utambuzi kwa wananchi hao walio katika kaya masikini.
CHANZO: HABARI LEO.

























0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa