UPUNGUFU wa matundu ya vyoo katika shule za msingi za Halmashauri ya
wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, imetajwa inaweza kusababisha mlipuko
wa magonjwa kutokana na baadhi ya shule wanafunzi wake kujisaidia ovyo.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo Hawa Ng’humbi
alisema wanaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wanaondoa tatizo
hilo.
Alikiri tatizo ni kubwa huku akibainisha kuwa matundu ya vyoo
yaliyopo ni 693 ambapo mahitaji yao 1,257 hivyo kuwa na upungufu wa 564.
Alisema ili kuondoa upungufu huo, ushirikiano wa pamoja unahitajika
baina ya wazazi na serikali kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira
mazuri yatakayokuwa rafiki kwao.
“Tunaendelea kuangalia jinsi ya kumaliza au kupunguza tatizo hili
maana ni kero kubwa watoto wanalazimika kwenda vichakani au nyumba za
jirani, ninaamini tukishirikiana tutafanikiwa,” alisema.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi , Sostenence Mbwilo alisema
wameshaanza kufanyia kazi changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment