JUMUIYA ya Waislamu wa Ahamadiyya mkoani Shinyanga imehimiza jamii kuishi kwa amani na upendo kwa kuzingatia sheria za Mungu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kiongozi wa jumuiya
hiyo, Shabani Luseza alisema wiki hii kutakuwa na mkutano wa jumuiya
unaolenga kuhubiri amani na upendo.
Alisema lengo ni kuwezesha wanadamu kufahamu sheria za kumjua Mungu
na kuondoa dhana potofu dhidi ya Uislamu kwa kuangalia matendo ya baadhi
ya watu au mataifa.
“Kuna baadhi ya watu wameweka fikra potofu juu ya Uislamu kwa
kuangalia mataifa ya nje matendo wanayofanya kinyume na Mungu na utu wa
mtu, kwani Uislamu hauwezi kuruhusu watu wake wakamwaga damu hivyo
jumuiya hii ina jukumu la kusimamia amani tuliyonayo mpaka sasa,”
alisema Luseza.
Alisema kaulimbiu ya ‘Upendo kwa wote bila chuki kwa yeyote’ inapaswa kuzingatiwa na jamii.
Alilaani vitendo vya uhalifu na mauaji kwa kusema unapomuua mtu
mmoja, umeua watu wote na ukimuacha hai mtu mmoja umewaacha hai wote.
Alisema wamekuwa bega kwa bega na serikali kuisaidia jamii kufanya
matendo mema na kufuata sheria za Mungu kuondokana na vitendo viovu.
Kuhusu mkutano, alisema utakwenda sambamba na mafundisho ya walezi na wazazi ili kuondokana na mila potofu.
Miongoni mwa mila hizo ni pamoja na ndoa za utotoni ambazo kwa mkoa wa Shinyanga umekuwa ukiongoza kwa asilimia 59.
Luseza alisema bado katika jamii upo upotoshaji juu ya Uislamu kuhusu
suala la kuruhusu wasichana wenye umri mdogo kuolewa. Alisema dini
hairuhusu na jumuiya imekuwa ikilipinga suala hilo.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment