WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kila mkoa unatakiwa kuunda
Kamati ya Amani, kama njia ya kudumisha amani na utulivu kwenye mikoa
yote nchini.
Alitoa mwito huo juzi usiku wakati akizungumza na viongozi wa dini wa
mkoa wa Dodoma na baadhi ya wazee maarufu wa mkoa huo aliowaalika
kwenye futari katika makazi yake mjini hapa. Alisema anatambua kuwa mkoa
wa Dodoma, uko shwari kwa sababu ya mshikamano uliopo baina ya viongozi
wa dini za Kiislamu na Kikristo.
“Nimegundua kuwa siri kubwa ya mkoa wa Dodoma kuwa na utulivu ni
kuwepo kwa kamati ya amani yenye viongozi mahiri, kwani sote tunatambua
kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kuwaimarisha watu kiroho,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ziko nchi zinatamani kuwa kama Tanzania kwa sababu wao, hawana uhakika wa kulala na kuamka salama asubuhi.
“Pamoja na yote sisi tuna uhakika wa asilimia 99 kulala usiku na kuamka salama asubuhi, kwa sababu ya amani iliyopo,” alisema.
Hadi sasa mikoa ambayo imekwishaunda Kamati za Amani ni Dar es
Salaam, Mwanza, Geita, Dodoma, Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga na Mbeya.
Akigusia mauaji ya hivi karibuni nchini, Waziri Mkuu aliwaomba
Watanzania kila mmoja kwa imani yake akemee kwa nguvu matendo hayo kwa
sababu yeye haamini kama yamefanywa na Watanzania ambao wamelelewa
kwenye misingi ya dini.
“Siamini kama kuna mtoto aliyelelewa kwenye misingi ya Uislamu
anaweza kuingia msikitini na kuwaua wenzake wakati wakimwomba Mungu. Na
wala siamini kama kuna mtoto aliyelelewa na kukuzwa Kikristo anaweza
kuingia kwenye nyumba ya ibada akakuta watu wanasali na kuamua kuwaua.
Ninawaomba tukemee kwa nguvu zote tabia hii,” alisema.
Aliwataka Watanzania wote wawe walinzi wa wenzao kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumlinda mwenzake.
Chanzo Gazei la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment