OFISA Elimu mkoani Shinyanga, Mohamed Kahundi, amewashauri wazazi
kusomesha watoto wao na si kuwakatisha masomo kwa ajili ya kuwaozesha
ili wapate mifugo, kwakuwa kufanya hivyo kunawanyima haki ya kupata
elimu na kuwajengea umasikini.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya kidato cha
nne katika shule ya sekondari Kom. Ushauri huo ulitokana na kuendelea
kuwepo kwa wazazi wanaokataa kusomesha watoto wao wa kike ili wawaozeshe
na kupata mifugo.
Kahundi alisema kwenye dunia ya sasa elimu ndio kila kitu katika
kumjenga mtoto kimaisha, hivyo ni vyema wazazi mkoani Shinyanga
wakabadili mitazamo yao hasi na kujikita kuwekeza elimu kwa watoto wao
watakaokuja kuwasaidia kimaisha baadaye.
"Ukisomesha mtoto ni sawa na kujiwekea hazina yako ya baadaye pale
utakapozeeka na kuishiwa nguvu za kufanya kazi, kwa sababu yeye ndiye
atakayekuja kugeuka kuwa mlezi wako na atakulea vizuri akiwa na elimu,”
alisema.
Aidha, aliongeza kuwa ni vyema sasa wazazi mkoani humu wakaacha
kuthamini mifugo kuliko utu wa mtu, bali wapende elimu na kusomesha
watoto wao ili hapo baadaye waje wale matunda ya elimu na kuwa na maisha
bora na kutokomeza umasikini.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Peter Kuguru, aliwataka wazazi
kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni na
kuwatimizia mahitaji yote, ili kuwaepusha na vishawishi ambavyo vimekuwa
vikikatisha ndoto zao.
Mkuu wa shule hiyo, Mwita Warioba alisema wanafunzi waliohitimu
masomo hayo ya kidato cha nne ni 144, wasichana wakiwa 60 na wavulana
84.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment