TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli, leo tarehe 12 Januari, 2017 amemaliza ziara ya siku mbili mkoani
Simiyu na kuanza rasmi ziara ya siku mbili mkoani Shinyanga na kuahidi
kuendelea kuulinda Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa nguvu zake
zote uliotokana na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12,1964.
Rais Magufuli amesema Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964
ndio yaliyosababisha kuwepo kwa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na
hivyo kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuna umuhimu mkubwa
kwa Watanzania kuuenzi na kuulinda kwa manufaa ya wananchi wote.
''
leo ni siku muhimu sana kwetu Watanzania kwa kuwa siku hii ya Januari
12,1964 miaka 53 iliyopita ndio siku yalipofanyika Mapinduzi
matukufu ya Zanzibar yaliyopelekea kuondolewa kwa utawala dhalimu wa kikoloni
na kupelekea kuzaliwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Tanzania
Bara na Zanzibara kuungana,hivyo tuna kila sababu ya kuienzi siku hii
muhimu'' amesema Rais Magufuli.
Akiwa Wilayani Maswa mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea
kiwanda cha kutengenezea chaki na kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa barabara
ya Mwigumbi hadi Maswa yenye urefu wa kilomita 50.3 kwa kiwango cha lami, Rais
Magufuli amewataka wananchi wa mkoa wa Simiyu kutumia barabara hiyo kujiletea
maendeleo.
Rais Magufuli ameupongeza mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza kwa
vitendo Sera ya Serikali ya awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda kwa ujenzi wa
kiwanda cha Chaki na kutoa wito kwa uongozi wa kiwanda hicho kuongeza
uzalishaji wa chaki ili ziweze kukidhi soko la nchi nzima badala ya mikoa kumi
ya sasa inayotumia chaki zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya viongozi wa serikali wenye
tabia ya kuwapangia bei ya mazao wakulima na kuwataka wawaache wakulima wauze
mazao yao kwa bei itakayowanufaisha wakulima kutokana na mazao yao tofauti na
ilivyo sasa ambapo mkulima amekuwa akipunjwa kutokana na bei ndogo anayolipwa
pindi anapouza mazao yake.
Akiwahutubia wananchi wa mkoa wa Shinyanga katika Uwanja wa
Kambarage alipoanza ziara ya siku mbili katika mkoa huo , Rais Magufuli
ameutaka uongozi wa mkoa huo, Wizara ya Viwanda pamoja na Wizara ya Kilimo,Mifugo
na Maendeleo ya Uvuvi kufuta mradi wa kiwanda cha kusindika minofu ya nyama cha
Triple S kutokana na mwekezaji huyo kukaa muda mrefu bila kiwanda hicho
kufanyakazi.
Rais Magufuli pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Shinyanga
kufuta leseni ya Mwekezaji aliyetaka kuchukua machimbo ya wafanyabiashara
wadogowadogo zaidi ya 15,000 katika eneo la Mwakitoliyo Wilaya ya Shinyanga
vijijini.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Shinyanga
12 Januari, 2017
0 comments:
Post a Comment