WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wametakiwa kuendelea kuifanya
sekta hiyo kuwa ya heshima zaidi tofauti na miaka ya nyuma ambapo
ilionekana kuwa ni sehemu ya watu waliokata tamaa.
Hayo yamesemwa mjini Mpanda na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Rafael Muhuga
wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wachimbaji madini wadogo
watakaonufaika na ambao hawatanufaika na Ruzuku ya Awamu ya Tatu ikiwa
ni maandalizi ya kuwajengea uwezo ili ruzuku hizo zitumike kama
ilivyokusudiwa kabla ya kukabidhiwa rasmi leo.
Alisema serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku
itakayowawezesha wachimbaji hao kununua vifaa vitakavyosaidia kwenye
shughuli za uchimbaji na kueleza kuwa, imedhamiria kuendelea kufanyia
kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ndogo ya madini nchini.
Alisema juhudi za serikali kuunga mkono shughuli za uchimbaji
zinaonekana wazi na kuzitaja baadhi kuwa ni pamoja na kutoa ruzuku
inayowezesha kupatikana kwa vifaa vya kisasa vya uchimbaji na uchenjuaji
madini, uanzishwaji wa vituo vya mfano vitakavyotoa mafunzo ya
teknolojia mbadala wa matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini
na kuboresha na kurahisisha utoaji wa leseni ndogo za madini ambapo
hivi sasa zinatolewa mikoani badala ya Dar es Salaam pekee.
Awali, akizungumzia Ruzuku ya Awamu ya Tatu, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe
alisema katika awamu mbili zilizopita serikali imeona baadhi ya
wanufaika wa ruzuku hizo wakifanya vizuri katika shughuli za uchimbaji
na hata takwimu za uzalishaji madini zimeanza kuongezeka.
Aliongeza kuwa katika awamu mbili zilizopita, zipo kasoro ambazo
serikali ilizibaini hivyo awamu ya tatu itatumika kuboresha kasoro hizo
na kuongeza kuwa, katika awamu ya tatu sehemu kubwa ya fedha zitatumika
katika kununulia vifaa ambavyo wazabuni watavisafirisha hadi katika eneo
la kazi na kuwapa mafunzo wanufaika ya namna ya kuvitumia na pia
mzabuni atatakiwa kutoa uhakikisho wa vifaa hivyo.
“Fedha zitapita Benki ya Maendeleo ya TIB, lakini Wizara ya Nishati
na Madini itasimamia mchakato wote, hadi vifaa kufikishwa eneo la kazi
na mnufaika kukabidhiwa. Vikundi vitakavyopaa ruzuku hii tutavisimamia
kuhakikisha kinakuwa na katiba za vikundi vyao na uongozi imara,”
alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment