WALINZI wa Kampuni ya Zeneth wanaolinda mgodi wa almasi wa Williamson
Diamond Limited uliopo Kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu mkoani
Shinyanga, wamevamiwa na wachimbaji wadogo maarufu kama Wabeshi zaidi ya
150 kwa kurushiwa mawe na kusababisha kifo cha mchimbaji mdogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo Novemba 20, mwaka huu saa 5 usiku katika eneo la
shimo namba nane ndani ya mgodi huo, ambako walinzi wa mgodi huo
walianza majibizano na wachimbaji wadogo hao.
Kamanda Haule alisema Wabeshi zaidi ya 150 walivamia eneo la mgodi
linalochimbwa na mgodi huo na kulindwa na walinzi kutoka Kampuni ya
Zeneth, ambako walianza kurushiwa mawe na kusababisha kifo cha Gile
Ikula (20), mkazi wa Kijiji cha Nyenze wilayani humo ambaye alikuwa
miongoni mwa Wabeshi.
Hata hivyo, kamanda alisema watuhumiwa wawili ambao ni walinzi
wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi ambao ni Fabian Bona (25) na
Paschal Patrick (27), huku watuhumiwa wanne ambao ni Lucas Gilungile
(24), Charles Kija (25), Joseph Tungu (28) na Charles Mluso (32)
wanashikiliwa kwa tuhuma za kuwajeruhi walinzi.
Alisema baada ya tukio hilo, baadhi ya Wabeshi waliubeba mwili wa
marehemu na kuupeleka kwenye taa ya shimo namba nane, na tayari
wanashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria pamoja na kufanya
mahojiano na watuhumiwa hao. Kamanda alitoa rai kwa wananchi hasa vijana
kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya migodini kwa lengo la kutafuta
mchanga wa madini ya almasi kinyume cha sheria.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment