WATU 40 wa Kitongoji cha Isumbi katika Kijiji cha Igung’hwa Kata ya
Kinaga katika Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, wamelazwa
katika Hospitali ya Wilaya hiyo baada ya kinachodaiwa kuwa ni kula
kiporo na mboga za majani aina ya mgagani.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kinaga, Paul Damasi alisema wananchi
waliolazwa katika Hospitali ya Mji wa Kahama ni wale waliokula kiporo
cha ugali na mboga za majani aina ya mgagani waliouita “mchicha.”
Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi katika msiba
uliotokea nyumbani kwa Salum Manyanda na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya
watu waliougua ghafla baada ya kula chakula hicho ni wanawake.
Ofisa Mtendaji wa Kata huyo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa
tano asubuhi baada ya waombolezaji kula chakula kilichobakia jana ya
siku hiyo huku akieleza kuwa wote waliougua ghafla walikimbizwa katika
hospitali ya Wilaya ya Kahama kupatiwa matibabu.
“Idadi ya watu haijafahamika ila nimepewa taarifa kuwa ni zaidi ya
wakinamama arobaini ndiyo waliokimbizwa katika Hospitali ya Mji wa
Kahama, msiba ulitokea Novemba 14, kama unavyojua vijijini bado kuna ile
tabia ya msiba unapotokea akinamama wanapika chakula nyumbani kisha
wanapeleka msibani.
“Ule ugali uliobaki siku ya kwanza ya msiba ulikosa mboga ikabidi
wakina mama waingie katika mashamba kuchuma mboga ambapo walipika mboga
aina mbili mrenda na mgagani uliodaiwa kuwa ni mchicha, sisi wanaume
tulikula ugali na mrenda akina mama wakala ugali na hiyo mboga ya
mgagani ndiyo chanzo cha tukio,” alisema.
Naye Joyce Samweli alilieleza gazeti hili kuwa wakati wakipeleka
chakula kingine katika msiba huo uliodumu siku mbili, alikutana na
akinamama wenzake waliougua ghafla ugonjwa huo wakionekana kukosa nguvu,
kuangua vicheko na kukimbia ovyo jambo lililoushangaza umati msibani.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment