Home » » WAFANYAKAZI BARRICK WAPINGA WARAKA SSRA

WAFANYAKAZI BARRICK WAPINGA WARAKA SSRA


na Ali Lityawi, Kahama
BAADA ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kusambaza waraka wa kuzitaka taasisi hizo sambamba na makampuni ikiwemo migodi ya madini kutowalipa mafao yao wafanyakazi wanaoacha kazi hadi watakapotimiza miaka 55, baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya African Barrick Gold Mines Ltd wameupinga waraka huo na kutishia kuacha kazi.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini wafanyakazi hao kutoka migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi iliyopo wilayani Kahama ambao wengi wao ni wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wameandika barua za kuacha kazi kwa madai kuwa uamuzi huo umetolewa bila kuwashirikisha.
Pamoja na SSRA kusambaza waraka kwenye mifuko hiyo nchini ikieleza ratiba ya kupita ikitoa elimu kwa wanachama juu ya mabadiliko yaliyojitokeza, wafanyakazi hao wamesema waraka huo una lengo la kuwadhulumu fedha zao ambazo huzichangia kila mwezi kutoka kwenye mishahara yao.
Walidai uamuzi wa kuchukua mafao yao baaada ya kufikisha miaka 55 hauko sawa kutokana na wengi wao kutokuwa na ajira za kudumu kwenye makampuni, kwani hufanya kazi kwa mikataba ya miaka michache na inapomaliza huondoka.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa, Omary Mzia, alisema suala hilo si la shirika lake bali ni agizo kutoka SSRA ambayo imetoa maelekezo hayo kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini.
Pamoja na maelezo hayo, takribani wafanyakazi 140 wiki iliyopita baada ya kupata waraka huo waliandiaka barua za kuacha kazi katika mgodi wa Bulyanhulu huku wengine jana walionesha mgomo wa kuendelea na kazi katika mgodi wa Buzwagi wakipinga hali hiyo.
Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya African Barrick Gold Mines, Necta Foya, alisema anakusanya takwimu za idadi kamili za wafanyakazi walioandika barua za kuacha kazi na taaarifa kamili atazitoa baadaye ingawa habari kutoka mgodi wa Bulyanhulu zimeeleza kuwa zoezi hilo limesitishwa.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa