na Ali Lityawi, Kahama
UONGOZI wa Wilaya ya Kahama, umetakiwa kulipatia ufumbuzi sakata la fidia kwa wakazi wa Kata ya Mwendakulima, waliopisha ujenzi wa mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mines.
Agizo hilo limetolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele, ikiwa ni hatua za kujaribu kulimaliza baada ya kumshinda aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, William Ngereja,
Baada ya kusomewa, taarifa ya wilaya, Masele alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kufuatilia madai ya fidia ya wananchi hao ili kuondoa kero hiyo iliyodumu miaka mingi.
Wananchi wa Kata ya Mwendakulima wapatao familia 230, walilipwa fidia na Barrick, lakini baadaye waliibuka na kuanza kudai upya kwa maelezo kuwa walipunjwa.
Katika madai yao, wananchi hao wanasema kuwa, kampuni hiyo ilikuwa ikiwalipa sh150 kwa mita ya mraba badala ya sh 500 hali ambayo ilifanya kamati mbalimbali zikaundwa kuchunguza ikiwemo ya aliyekuwa Naibu Waziri, Adamu Malima ambaye alitoa siku 90 kwa Serikali ya wilaya ya Kahama pamoja na mgodi, kumaliza tatizo hilo bila mafanikio.
Malima baada ya kutoa agizo la kuunda kamati ya kumaliza mgogoro uliokuwepo baina ya wakazi hao na mwekezaji huku akiagiza serikali ya wilaya ihakikishe inasimamia, aliondoka bila kutoa majibu ya kuridhisha juu ya ahadi ya siku tisini.
Hata hivyo, pamoja na Masele kuagiza wananchi hao walipwe madai yao, Mkuu wa wilaya, Mpesya, alisema ulipwaji wa fidia hizo una changamoto nyingi ikiwa ni kukosa ukweli wa madai hayo kutokana na baadhi ya vikundi kujipachika kudai fidia wakati walengwa halisi waliishalipwa na kuondoka.
Pamoja na hali hiyo, Masele alisema kuwa, Barrick katika migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu iliyopo wilayani Kahama, haiwanufaishi wananchi wa eneo hilo kutokana na mrahaba wanaolipa katika halmashauri wa dola laki mbili kila mwaka kuwa ni kiasi kidogo kisicholingana na uzalishaji mkubwa wanaofanya.
Alisema, tayari ameshaandaa utaratibu wa kukutana nao ili kuongeza kiasi hicho na kutoa mfano kwa wananchi wa Nyamongo wanavyonufaika na mgodi wa North Mara kwenye huduma za kijamii tofauti na Kahama wenye migodi mikubwa miw`ili inayomilikiwa na Barrick.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment