Home » » POLISI YAMNASA ALIYEMTISHIA KIFO LEMBELI

POLISI YAMNASA ALIYEMTISHIA KIFO LEMBELI

na Ali Lityawi, Kahama
HATIMAYE Jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga limefanikiwa kumnasa mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na kutoa vitisho vya kutaka kumuua Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli (CCM).
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umebaini kunaswa kwa mtu huyo ambapo hapo awali kulikuwa na madai yaliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kahama na mbunge huyo akidai kupokea ujumbe wa simu ya mkononi kwa mtu asiyefahamika akisema kama ataendelea kupambana na mafisadi kifo kinamsubiri.
Vitisho hivyo vya kifo kwa mbunge huyo ambavyo vilitoka kwenye vyombo vya habari, viliifanya polisi kuanza uchunguzi hadi juzi walipofanikiwa kumkamata mtu huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla alikiri kukamatwa kwa mtu huyo aliyegoma kumtaja jina kwa kuhofia kuvuruga upelelezi wao, wakidai bado wapo kwenye uchunguzi mkubwa wa kutaka kubaini kama kuna mtandao wa washirika wengine.
Habari zinaeleza kuwa mtu huyo alikamatwa akiwa na simu iliyokuwa na ujumbe mbalimbali aliokuwa akimtumia mbunge huyo.
Akizungumza kwa simu ya mkononi kutoka Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Kahama, Lembeli alithibitisha kupatiwa taarifa ya kukamatwa kwa mtu huyo, lakini alisema hawezi kuzungumza lolote bali anawaachia suala hilo polisi, huku akiwataka kufanya kazi yao kwa mujibu wa taratibu zao.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa