Home » » ASILIMIA 48 YA WANAWAKE WAFANYIWA UKATILI

ASILIMIA 48 YA WANAWAKE WAFANYIWA UKATILI

Na Sam Bahari, Shinyanga
ASILIMIA 48 ya wanawake wenye ndoa hufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa kulazimishwa na waume zao kufanya tendo la kujamiiana bila ridhaa yao.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Dk. Grace Mallya, katika mkutano wa kuwasilisha na kuhamasisha viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kuhusu mwongozo wa kisera na mwongozo wa sekta ya afya.

Aidha, alisema utafiti uliofanywa nchini mwaka 2009 na kuzinduliwa Agosti, 2011, ulibaini robo tatu ya watoto walio na umri chini ya miaka 18 wameathirika na ukatili mbalimbali wa kimwili waliofanyiwa na ndugu zao, walimu pamoja na viongozi wenye mamlaka kwa jamii.

Alisema pia utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 30 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 13 na 24 na asilimia 14 ya wanaume wenye umri kati ya miaka 13 na 24 waliripotiwa kuathirika na ukatili wa kulazimishwa kufanya tendo la kujamiiana na wanaume kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Alisema matokeo ya utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 32 ya watoto wa kike wenye umri wa chini ya mwaka mmoja walifanyiwa ukeketaji na asilimia 13 ya wasichana walifanyiwa ukeketaji wakiwa na umri wa miaka 13.

“Idadi ya wanawake wenye umri wa miaka mitano waliofanyiwa ukeketaji iliongezeka kutoka asilimia 34 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 39 kinyume na mkataba wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Dk. Mallya.

Alisema ilibainika mila potofu kama vile ukeketaji unaofanywa kwa wanawake na baadhi ya jamii nchini ni vitendo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa