Home » » VIJANA CCM WAHOFIA KUKATWA MAJINA YAO

VIJANA CCM WAHOFIA KUKATWA MAJINA YAO

na Ali Lityawi, Kahama
VUGUVUGU la uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) likizidi kupamba moto, hofu imetawala kwa wagombea vijana wilayani Kahama kukatwa majina yao huku baadhi yao wakidaiwa kuanza kampeni kabla ya uteuzi.
Baadhi ya wagombea wamemtuhumu mdogo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu, Catherine Dalali, anayeomba nafasi ya Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia wilayani kuanza kampeni kabla ya uteuzi kwa kupita vijijini hali ambayo wagombea wenzake wameanza kuwa na mashaka ya kukatwa majina yao.
Mmoja wa wagombea hao, Robert Kapera, ambaye kipindi kilichopita alikuwa mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya alidai kushangazwa kuona wenzie wakifanya kampeni kabla ya uteuzi hali ambayo imewafanya kujenga mashaka ya kuwapo kwa uteuzi wa siri.
Kapera alisema inakatisha tamaa kuona CCM haiwapi nafasi vijana tofauti na wale wa upinzani ambao vijana wamepewa nafasi kubwa ya uongozi na ndiyo maana vyama hivyo sasa vina nguvu ya damu changa tofauti na huku walikong’angania wazee kushika madaraka huku wengi wao wakiwa hawana elimu ya kutosha tofauti na wapinzani waliojaza wasomi.
Kufuatia hali hiyo Kapera aliyegombania nafasi ya Halmashauri kuu ya Taifa kupitia wilayani Kahama alisema hali inakatisha tamaa na kama haitadhibitiwa mwenendo wa chama hicho huko mbele utakuwa ni mbaya kwa kuwa vijana wengi watazidi kukimbia na kwenda kule wanakoheshimiwa na ndiyo utakuwa mwisho wa utawala wa CCM.
Hata hivyo Dalali anayelalamikiwa na wagombea wenziwe aliliambia gazeti hili kuwa madai hayo si ya kweli na kudai anahitaji kulindwa kwa hilo kwani yeye hajaanza kampeni za kutafuta kura kwa wapiga kura huko vijijini.
Dalali alisema yeye anavyojua ameomba nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia wilayani na hajaanza kampeni hivyo wanaomzushia lengo lao ni kumdhoofisha katika nafasi yake hiyo.
Akizungumzia hali hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama,Michael Bundalla, amewaonya vikali wagombea wote walioomba nafasi hizo kuacha kufanya kampeni kabla ya kupewa barua za uteuzi.
Bundalla alisema kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu hivyo yeyote atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa