na Ali Lityawi, Kahama
SAKATA la Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kumkwida na kumuondoa kwenye foleni ya
chakula Diwani wa Nyihogo, Amos Sipemba (CHADEMA), limeingia katika sura mpya
baada ya diwani huyo kudhamiria kulifikisha suala hilo katika vyombo vya
sheria.
Akizungumza na
Tanzania Daima jana, Diwani huyo alisema anadhamiria kuchukua hatua hizo dhidi
ya mkuu huyo wa wilaya kutokana na kumvunjia heshima mbele ya kadamnasi na
kwamba alitegemea baada ya Mpesya kutambua kosa lake angelimuomba radhi, lakini
hilo halikutokea.
Alisema
hakutarajia siku hiyo kama angekumbana na kadhia hiyo kutoka kwa kiongozi
ambaye ofisi yake ilimuandikia barua ya kumuomba kujumuika katika ziara ya
waziri mkuu kumuondoa pasipo kutumia ustaarabu kwenye mstari wa kwenda kupata
chakula cha mchana kwa madai kuwa amekiuka utaratibu.
Aidha,
alibainisha kitendo hicho ambacho kimewadhalilisha pia wapigakura wake tayari
amelifikisha katika chama chake kwa ajili ya ushauri zaidi.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mpesya, alisema alichukua uamuzi huo kutokana
na diwani huyo kuvunja utaratibu wa kwenda kuchukua chakula.
Katika hatua
nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Kahama, Juma Ntahimpera, amesema
chama hicho kinatarajia kufanya harambee kubwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya
wilaya itakayofanyika Septemba 30 mwaka huu katika Kata ya Bulyanhulu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment