Home » » SITTA AWATIBUA WAZEE SHINYANGA

SITTA AWATIBUA WAZEE SHINYANGA



Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
BAADHI ya wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, wametishia kuandamana kupinga kauli zinazoendelea kutolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, kwa niaba ya wenzake, mzee Shomvi Ibrahimu, alisema wazee hao walisema baadhi ya kauli zinazotolewa na Sitta, haziwezi kukubaliwa kwa sababu zinalenga kukivuruga chama.

Alizitaja kauli hizo kuwa ni pamoja na aliyoitoa akiwa wilayani Karagwe, Kagera, alipokuwa akizungumza na wajane wilayani humo, ambapo alisema Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ni ndoto.

Kwa mujibu wa mzee huyo, kauli hiyo ya Sitta inampinga Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amekuwa akihimiza uwepo wa kauli hiyo.

Kauli nyingine aliyoitaja ni ile aliyowahi kuitoa Mjini Mbeya akiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kwamba Serikali lazima iombe radhi kwa Watanzania, kutokana na mgao wa umeme uliokuwa ukiendelea mwaka jana.

Pamoja na kutoridhishwa na kauli za Waziri Sitta, alisema wazee hao wameunda timu atakayoiongoza yeye (Mzee Shomvi), ili wapeleke malalamiko yao kwa Katibu Mkuu CCM, Wilson Mukama, kuonyesha jinsi wasivyoridhishwa na kauli za waziri huyo.

Aliwataja wajumbe wengine watakaokuwa katika timu hiyo, kuwa ni Alphonce Bundala, Masanja Njile, Maimuna Salehe na Peter Zakaria.

“Kauli hizi za kuchanganya anazozitoa Sitta hatuwezi kumvumilia, kwa sababu inaonekana yeye anaajenda moja ya kukibomoa chama.

“Yeye ni waziri katika Serikali inayotawala, sasa anapoanza kusema maneno yanayoonyesha anakwenda kinyume na msimamo wa chama, sisi kama wana CCM hatuwezi kumvumilia kamwe.

“Kwa mfano, hivi majuzi alikuwa kwenye mahafali ya pili ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Kwema, iliyoko Kahama na akakaririwa akisema, CCM inatia aibu kuachia ufisadi kujichimbia ndani ya chama.

“Kauli hii inaonyesha ni kwa jinsi gani asivyokuwa na imani na chama chake, kwani kitendo cha kuwaambia watoto hao mambo hayo, maana yake ni kwamba alikishitaki chama chake kwa wanafunzi ambao si wanachama wa CCM.

“Sisi tunajua maana yake anajiandaa katika uchaguzi mkuu ujao, kwani tunajua anataka kugombea wakati wa uchaguzi huo na kama akishinda Lembeli (Mbunge wa Kahama, James Lembeli) awe Waziri Mkuu wake.

“Kwa kifupi sisi hatumzuii kugombea, yeye agombee tu ila anachotakiwa ni kufuata utaratibu na awaonyeshe Watanzania kwa kauli na kwa vitendo, kwamba akipewa nchi ataweza,” alisema mzee huyo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa