Home » » JINA LA KHAMIS MGEJA HATARINI KUKATWA CCM

JINA LA KHAMIS MGEJA HATARINI KUKATWA CCM

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, anayewania nafasi hiyo, Khamis Mgeja, jina lake liko hatarini kukatwa. Mkakati huo umedaiwa kuwa ni moja ya mikakati ya baadhi ya vigogo walioko katika harakati za kupanga safu zao zitakazowawezesha kushiriki ipasavyo kampeni za kumpata Mgombea Urais wa mwaka 2015 kupitia CCM.

Chanzo chetu kimesema kuwa, wanaoongoza mkakati huo ni wanaompinga Mgeja kwa kuwa hayuko katika kambi yao.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, hivi sasa vigogo hao wanafanya kila aina ya ushawishi kwa wajumbe wa ngazi za juu, ili kuhakikisha jina la Mgeja linakatwa na kubakizwa mgombea wanayemtaka wao, kwa kuwa atawasaidia wakati wa kampeni hizo.

Mmoja wa wajumbe wa CCM mkoani Shinyanga, alisema ili kufanikisha mkakati huo awali vigogo hao walimshawishi mwanachama mmoja, ili aweze kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, kwa lengo la kumng’oa Mgeja, katika nafasi hiyo.

“Kuna vikao vinafanyika katika maeneo mbalimbali mjini hapa na taarifa hizi hata baadhi ya watu wamezifikisha TAKUKURU, ili iweze kuwafuatilia maana kuna madai ya kumwaga fedha kwa wajumbe na hili linafanyika kwa sababu watu wanapanga safu zao za viongozi.

“Kibaya zaidi aliyekamiwa sana ni Mgeja, huyu inashinikizwa jina lake lisirudi kabisa, maana ndiye anayeogopwa na baadhi ya vigogo hao wa kitaifa, wanafanya kila juhudi akatwe na tayari wamemuandaa mtu wao ili achukue nafasi hiyo, kwa sababu wanaamini atawasaidia,” alisema Samwel Steven mkazi wa Ibadakuli.

Kwa upande wao baadhi ya wazee wa CCM waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi, walielezea masikitiko yao kuhusiana na mikakati hiyo ambayo walisema haina maslahi yoyote kwa chama bali kwa watu binafsi.

“Iwapo kweli haya tunayoyasikia yatakuwa ni ya kweli, basi viongozi wetu hawakitendei haki chama chetu, mara kwa mara tunaelezana wanachama tudumishe ushirikiano na mshikamano, lakini wao wanaonekana kutenda tofauti na wanafanya kampeni chafu zitakazosababisha tugawanyike, hii ni hatari,” alisema mwana CCM huyo kwa sharti la kutotaja jina.

Kwa upande wake, Mkazi wa Kata ya Shinyanga Mjini, Juma Amani, alisema kuwa ili kuondoa malumbano yasiyo na tija ndani ya chama, ni vizuri vikao vya mwisho vya uteuzi vikawa makini katika kuteua majina ya wagombea.

“Mimi nashauri ni vyema vikao vya uteuzi vikapuuza propaganda zozote chafu zinazoweza kusababisha CCM kupoteza watu muhimu na makini, hii itasaidia kuepusha mambo ambayo yamewahi kutokea huko nyuma, maana baadhi ya wana CCM waliobaini kuchezewa mchezo mchafu kama unavyoandaliwa sasa walikimbilia vyama vya upinzani, mfano Dk. Slaa,” alisema Juma.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa