Home » » KIWANDA KILICHOTELEKEZWA SHINYANGA CHAPATA MWEKEZAJI

KIWANDA KILICHOTELEKEZWA SHINYANGA CHAPATA MWEKEZAJI

Na Sam Bahari, Shinyanga
HATIMAYE kiwanda cha nyama cha mjini Shinyanga kimepata mwekezaji, ambaye ni Kampuni ya Triple S Ltd, baada ya kutelekezwa na Serikali kwa zaidi ya miaka 36.

Akizungumza mjini hapa jana, Mtaalamu wa Vyakula, Charles Malobana, alisema ukarabati wa kiwanda hicho umefikia hatua ya kuridhisha.

Alisema wawekezaji walionunua kiwanda hicho ni wazalendo na walianza kukifanyia ukarabati Juni, mwaka huu na kinatarajiwa kuanza kazi kabla ya Desemba 30, mwaka huu.

Alisema kiwanda hicho kitakapoanza kazi ya uzalishaji kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 250 kwa siku na kitaajiri wafanyakazi 50.

Alisema kukamilika kwa ukarabati na kuanza kazi kwa kiwanda hicho kutatoa fursa kwa wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao.

Alisema wateja wa nyama na bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho watatoka ndani ya nchi pamoja na wateja kutoka nje ya nchi.

Alisema licha ya uzalishaji wa nyama pia kutakuwa na uzalishaji wa bidhaa nyingine kama vile ngozi, kwato, mifupa na mbolea ya samadi itakayouzwa kwa wakulima.

“Katika kuhakikisha kunakuwapo kwa soko la uhakika, uongozi wa kiwanda hicho unafanya juhudi za makusudi kuzishawishi kampuni zinazochimba madini nchini kununua nyama hizo,” alisema Malobano.

Alizitaja nchi ambazo kiwanda hicho kinatarajia kuziuzia nyama kuwa ni Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC), Afrika ya Kusini na Arabuni.

Alisema wakulima na wafugaji wanaoishi kandokando ya kiwanda hicho watanufaika na huduma za ugani, ikiwamo za kuogeshewa na chanjo kwa mifugo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa