Home » » MAHITAJI YA MKONGE YAONGEZEKA, UZALISHAJI WAKE WAPUNGUA

MAHITAJI YA MKONGE YAONGEZEKA, UZALISHAJI WAKE WAPUNGUA

Na Sam Bahari, Shinyanga

WAKATI mahitaji ya mkonge duniani yameongezeka hadi kufikia tani milioni 11 kwa mwaka, lakini uzalishaji wake umeshuka hadi kufikia tani 300 kwa mwaka.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Ofisa Mipango na Utafiti wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Hassan Kibarua, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Alisema TSB ina mkakati wa kufufua kilimo cha zao la mkonge kutokana na kuongezeka kwa bei ya zao hilo na kuongezeka kwa mahitaji ya mkonge duniani.

Alisema mkonge unastahimili ukame lakini unadumu shambani kwa kipindi cha miaka 10 hadi 25 na hutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwamo kutengenezea magunia, magari, ndenge, meli, kamba na ujenzi wa nyumba za kisasa za bei nafuu kwa kutumia teknolojia mpya.

Alisema TSB imeanzisha mkakati maalumu wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo katika Halmashauri zote katika Mikoa ya Tanga, Lindi, Pwani, Mtwara, Mara, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Singida na Tabora.

Alisema sera ya kilimo cha mkonge na mfumo wa uendelezaji wake ulianza mwaka 1960 katika eneo la Kabuku wilayani Handeni mkoani Tanga.

Alisema kuanzishwa kwa mfumo wa wakulima wadogo wa mkonge katika kipindi hicho, haukufanikiwa kutokana na wananchi kutoshirikishwa kikamilifu katika mpango huo.

Alisema mkonge hulimwa kwa kuchanganywa na mazao mengine ya chakula kwa msimu kama vile mahindi, kunde, njugu, maharage, alizeti, njegere na karanga.

Alisema lengo la kuanzishwa kwa mpango wa kilimo cha mkonge kwa wakulima wadogo ni kuhakikisha sekta hiyo inamilikiwa na wakulima wadogo, kwa ajili ya kuboresha na kuinua uchumi wao.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa