Na Antony Sollo, Kahama
HATIMAYE aliyekuwa mmoja wa waombaji wa nafasi
ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, James Lembeli, amempongeza mgombea wa
nafasi hiyo mkoani hapa, Hamis Mgeja, kwa kuteuliwa kwake kutetea nafasi hiyo.
Lembeli aliyasema hayo jana mjini Kahama, katika mkutano wa uchaguzi wa
viongozi wa ngazi mbalimbali unaoendelea ndani ya chama hicho nchini kote.
Lembeli akiwa na furaha, tofauti na siku nyingine, aliushangaza umati uliokuwa
katika ukumbi huo, akiwamo Mkuu wa Wilaya hiyo, Benson Mpesya.
“Nakupongeza sana ndugu yangu Mgeja, chama kimekuamini na kuthamini utendaji
wako na uaminifu wako na hali hii ndiyo iliyopelekea kuteuliwa kwako ili
uitetee nafasi yako ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
“Mimi mwenyewe nimeridhika kwa jina langu kutorudishwa na Halmashauri Kuu ya
CCM Taifa kugombea nafasi hii. Natamka wazi, sina kinyongo ninayaheshimu
maamuzi ya chama,” alisema.
Kwa upande wake, Mgeja alimshukuru Mungu na kuipongeza NEC iliyokaa hivi
karibuni mjini Dodoma chini ya Rais Jakaya Kikwete na kupitisha jina lake ili
aweze kuitetea nafasi yake.
Mgeja aliwapongeza wagombea nafasi mbalimbali waliojitokeza kwa wingi kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi katika mkoa huo na kusema kuwa wagombea wote
waliopitishwa na wale ambao hawakupata nafasi hizo wote ni sawa na hakuna aliye
bora zaidi ya mwenzake.
“Nafasi zilikuwa ni chache, nawaomba msikate tamaa, kipindi hiki tunahitaji upendo,
umoja na mshikamano wa dhati ndani ya chama,” alisema.
Mgeja pia alimpongeza Lembeli kwa kuonyesha uzalendo na kutanguliza maslahi ya
chama mbele kwa kukubali uamuzi uliotolewa na vikao vya chama ngazi ya Taifa.
“Kitendo alichofanya Lembeli ni kitendo cha uungwana na kinafaa kuigwa na
wanachama mbalimbali nchini, hasa wanaokitakia mema Chama Cha Mapinduzi,”
alisema Mgeja.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment