Na Editha Edward, Shinyanga
WAZAZI na walezi wenye watoto ambao niwalemavu
wa ngozi (albino), wametakiwa kuachana na tabia ya kuwatelekeza watoto hao
katika vituo maalumu vya kulelea watoto.
Hali hiyo imewafanya baadhi ya watoto hao kutofahamika wanaishi maeneo gani na
mahali walipozaliwa na kwamba, wakati wa likizo watoto hao huendelea kubaki
vituoni.
Hayo yalielezwa jana na Mwanaharakati Josephat Torner, anayetetea masuala ya
walemavu wa ngozi nchini katika Kituo cha Buhangija wilayani Shinyanga.
Torner alikuwa akikabidhi msaada wa magodoro 20 yenye thamani ya zaidi ya Sh
milioni moja, kwa kituo hicho kinacholelea watoto wenye ulemavu wa aina
mbalimbali.
“Mtoto akizaliwa anakimbizwa shule maalumu kisha wazazi wao wanaendelea na
maisha bila ya kuja kuwajulia hali watoto wao, huku wakidiriki kuhama maeneo.
“Inasikitisha mtoto kutomjua mama yake na wala kufahamu sehemu aliyozaliwa hata
wakati wa likizo wanaendelea kuishi kituoni kwa imani akirudi katika familia
atauwawa,” alisema.
“Kwa sasa suala hili limekuwa janga la kitaifa kwa sababu kila mkoa hali hii
ipo. Huu ni wakati wa kujiuliza kwa nini litokee sasa na sio zamani?,” alihoji.
Alisema, tangu kuanza kwa mauaji ya walemavu wa ngozi mwaka 2007 taifa limepata
doa kubwa, kwa watu wenye ulemavu huo ambapo takribani watu 72 walipoteza
maisha na watu 28 wakijeruhiwa.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Jesca Kagunila alisema
msaada huo ni mkubwa, kwani mtoto mwenye ulemavu anastahili kulala sehemu nzuri
kama mtoto mwingine.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment