Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MBUNGE wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora, Dkt. Hamis Kigwangala, ametangaza
kuunga mkono dhamira ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CHADEMA, Bw.
Zitto Kabwe, ya kutangaza kuwania urais mwaka 2015.
"Naunga mkono Bw. Zitto kwa dhamira yake ya kutaka kuwania uongozi wa juu
kabisa katika nchi yetu japokuwa yuko CHADEMA na mimi niko
CCM," alisema Dkt. Kigwangwala.
Dkt. Kigwangwala alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia wanafunzi wa
Sekondari ya Shinyanga, iliyopo wilayani Kishapu mkoani hapa, wakati wa
mahafali ya 46. Katika mahafali hayo, Dkt. Kigwangwala alikuwa mgeni rasmi.
Mbunge huyo alisema vijana wanaomaliza masomo yao wasipokuwa na malengo ya kuwa
viongozi wa nchi itakuwa hatarini kujikuta ikikosa vijana makini.
Hapo ndipo alipotolea mfano Bw. Zitto, akisema alisoma naye shule moja, ambapo
tangu akiwa masomoni alikuwa na ndoto ya kuwa kiongozi.
“Binafsi nampongeza kijana mwenzagu Zitto (Kabwe), maana tangu tukiwa shuleni
alikuwa na malengo ya kuwa kiongozi, sasa hivi ametangaza nia yake ya kutaka
kuwania urais wa Tanzania mwaka 2015, ameniwahi hata mimi natamani siku
moja nitakuwa rais, lakini leo hii hapa sitangazi nia hiyo,” alisema Dkt.
Kigwangwala na kuongeza;
“Muda wake bado, ipo siku nitatangaza dhamira hiyo, akijitokeza kijana
nitamuunga mkono...kwa hiyo namuunga mkono Zitto kwa dhamira yake ya kutaka
kuwania uongozi wa juu japo naelewa hawezi kutushinda CCM.”
Ili taifa liendelee kupata viongozi, Dkt. Kigwangwala alisema hakuna
sababu ya vijana waliopo mashuleni kubaki na dhana kuwa masuala ya siasa
yanahusu wanasiasa waliopo madarakani au watu wazima peke yake, badala yake
waanze kujiwekea malengo yatakayowawezesha kushika uongozi wa nchi.
Aliwataka vijana watakaobahatika kuingia katika siasa na kupata nafasi za
uongozi kujiepusha na siasa za makundi ambazo hivi sasa zinaitafuna nchi.
“Epukeni makundi yanayohujumu Serikali na hatimaye kutaka uongozi wa nchi yetu,
hakikishesni mnawakwepa wanasiasa wa aina hiyo, maana hawafanyi siasa kwa
malengo ya jamii, hawafanyi siasa kwa malengo ya umma wanafanya siasa kwa
malengo ya kutunisha matumbo yao,"alisema Dkt. Kigwangala.
Kwa upande mwingine, Dkt. Kigwangala alijitolea kuichangia shule hiyo msaada wa
vitanda vyenye thamani ya sh. milioni tatu, kabati mbili kwa ajili ya chumba
cha wanafunzi wasioona, na vifaa mbalimbali vya michezo.
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment