Wajumbe wa kamati ya Ulinzi
na usalama ya Mkoa wa Shinyanga wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa
KASHWASA jinsi mradi huo unavyofanya kazi.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya
kusambaza maji Kahama na Shinyanga(KASHWASA), Ndg.Clement Kivegaro akiwaonesha
wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Shinyanga chanzo cha Maji
kilichopo ziwani ambacho ni "Open channel" kutoka ziwa
Viktoria.kamati hiyo ilitembelea chanzo hicho Jumatatu hii huko Ihelele
wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi
na usalama wakiendelea kuona kazi zinazofanyika ili kuhakikisha wananchi
wanaopata maji kutoka chanzo hicho yanakuwa salama kwa matumizi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Mhe.Rufunga akipanda tanki la maji linalosambaza maji ya Ziwa Viktoria katika
miji ya Shinyanga na Kahama,mbele yake akiongozwa na Mkurugenzi wa KASHWASA
Ndg.Kivegaro
Mamlaka ya kusambaza Maji katika miji ya Shinyanga na Kahama
(KASHWASA) inayoendesha mradi mkubwa wa maji ambayo chanzo chake ni Ziwa
Viktoria,ina uwezo wa kusambaza na kusafirisha maji kwa mikoa mitano kutokana
na uwezo mkubwa wa mashine za kusukuma maji pamoja na wingi wa maji.
Hali hiyo imebainika baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa
wa Shinyanga ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa Mhe.Ally N.Rufunga,
kutembelea Ofisi kuu za mamlaka hiyo zilizopo Ihelele wilaya ya Misungwi na
Jumatatu ya wiki hii,kuona shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa maji
kutoka kwenye chanzo cha Ziwa Viktoria.
Changamoto kubwa iliyobainishwa na Mkurugenzi wa KASHWASA
Ndg.Clement Kivegaro wakati akisoma taarifa ya mamlaka ni uchache wa watumiaji
wa maji ambapo alisema kwa sasa mamlaka inasambaza maji kwa asilimia 13 tu ya
uwezo wake hivyo inalazimika kuwasha pampu moja tu ya kusukuma maji, kati ya
pampu tatu zilizopo.
Kamati iliweza kutembelea mradi huo kwa muda wa zaidi ya saa 2 na
kupata maelezo ya kina juu ya uendeshaji na usambazaji wa maji,ambapo mradi una
uwezo wa kuzalisha maji kwa kiwango cha "cubic metres" 120,000 kwa
siku.
Mradi unauza maji kwenye mamlaka ya maji Shinyanga( SHUWASA),
mamlaka ya maji Kahama (KUWASA) na jumla kamati 45 za maji vijijini.
Mhe.Rufunga wakati akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo
amesema, lazima serikali ihakikishe wilaya ya Kishapu nayo inapata maji
ili kupanua wigo wa watumiaji wa maji, na kuhamasisha mikoa mingine kununua
maji kutoka chanzo hicho kwa sababu pamoja na uwezo mkubwa wa mradi huo,bado
haujatumika ipasavyo kulingana na uwezo wake unaokadiriwa kulisha mikoa zaidi
ya mitano.
Amesema pia kazi ya serikali ni kutafuta fedha ili kushughulikia
matatizo yaliyo ndani ya uwezo wa Mkoa kama kuweka mazingira mazuri kwa
watumishi wa Mamlaka hiyo kwani chanzo hicho kipo mbali na huduma muhimu kama
hospitali, shule na maeneo ya biashara.
Magdalena Nkulu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shinyanga
0 comments:
Post a Comment