IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa hosteli kwenye shule
za sekondari wilayani Kahama na vijana kutopata elimu ya afya ya uzazi ni
chanzo cha wasichana wengi kukatisha masomo kwa sababu za ujauzito.
Hayo yalielezwa na Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri
ya Mji wa Kahama, Perpetua Maige, wakati wa mkutano wa uhamasishaji wa Afya ya
Uzazi kwa vijana iliyohusisha walezi, viongozi wa mkoa na Halmashauri ya Mji wa
Msalala za wilayani Kahama, iliyofanyika mjini Shinyanga.
Maige alisema tatizo hilo ni kubwa maeneo ya
vijijini kutokana na wanafunzi wa kike kulazimika kupanga mitaani huku
ikiwalazimu kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni, kitendo ambacho huwaingiza
majaribuni kwa kutongozwa na wanaume.
“Kutokana na mazingira magumu ya kujisomea hasa kwa
mtoto wa kike imesababisha kwa mwaka huu hadi kufikia mwezi huu tayari mabinti
22 wameacha shule baada ya kubainika ni wajawazito, hiyo ni kwa watoto walio
shule za halmashauri ya mji,” alisema Maige.
Aidha, kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Issac Njalu, akiwasilisha mada za afya ya uzazi
kwa vijana, katika mkutano huo uliofadhiliwa na UNFPA alisema wasichana wengi
huingia katika matendo ya ngono pasipo kujiamini.
Alisema hilo ni janga kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa
kwa watoto wa kike kukatisha masomo kwa kupachikwa mimba ama kutopata elimu
kutokana na kuozeshwa katika umri mdogo.
Njalu alisema kuwa ndoa za utotoni hutokea miongoni
mwa wasichana ambao hawajaelimika na kutofikiwa na taarifa mbalimbali za afya
ya uzazi wa mpango, hasa kwa maeneo ya vijijini, ambapo wanajiingiza katika
masuala ya ngono kwa kutojiamini na mikakati ya makubaliano inakuwa haifanyiki.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment