Home » » Wakala wa vipimo yatangaza kiama kwa wafanyabiashara

Wakala wa vipimo yatangaza kiama kwa wafanyabiashara

MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa Shinyanga, Luppy Shirima, amewatangazia kiama wanafanyabiashara ambao wamekuwa wakitoa vipimo vya uongo katika bidhaa za wananchi. Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi wa mkoa huo kuwa makini pindi wanapokuwa wananunua bidhaa zilizofungashwa kwa kuhakikisha zina vipimo halisi kulingana na mahitaji yao.

Kauli hiyo imetolewa jana wilayani Kahama na Meneja huyo wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu, katika zoezi la ukaguzi na upigaji wa chapa katika mizani.

Alisema kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ambao si waaminifu, hasa wa mabucha ya nyama ambao wamekuwa wakitumia vipimo ambavyo si sahihi katika mizani yao.

“Nimetoa agizo kwa maduka yote ya jumla yahakikishe yanakuwa na mizani halali iliyoidhinishwa na wataalamu ili mteja anaponunua bidhaa aweze kupima kama ujazo wa bidhaa ni halisi,” alisema Shirima.

Shirima alisema kuwa wamekuwa wakikabiliana na changamoto kupuuza faini inayotozwa na WMA kuwa ni ndogo ambayo ni kati ya Sh 10,000 na 40,000, hali inayowafanya warudie makosa huku wakijua wana uwezo wa kuyalipa.

Alisema kutokana na hali hiyo, WMA ipo katika mchakato wa kuandaa sheria mpya za vipimo ambayo itawasilishwa bungeni kwa hatua zaidi.

Chanzo: Rai

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa