Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N.Rufunga
Katibu Tawala Mkoa wa
Shinyanga Dkt. Anselm Tarimo
Serikali Mkoani
Shinyanga imetoa rai kwa watendaji wote hususani Wakurugenzi wa Mamlaka za
serikali za mitaa kusimamia kazi za barabara kwa kufuata sheria na kanuni
kinyume chake serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji ambao watashindwa
kusimamia miradi kwa umakini.
Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Ally Rufunga ametoa rai hiyo jana kwenye kikao cha Bodi ya Barabara
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mhe.Rufunga amesema, usimamizi
mbovu unaisababishia serikali gharama za matengenezo zisizo za lazima,hivyo
kuathiri shughuli za miradi mingine ya maendeleo pamoja na kuhatarisha usalama
wa watumiaji wa barabara.
Amesisitiza watendaji
kutumia wakandarasi wanaostahili kielimu na vifaa vya kutosha, kuepuka rushwa
na Wakurugenzi wote na Katibu Tawala Mkoa, kufanya ukaguzi wa barabara ili
kujiridhisha utekelezaji wake.
Amesema pia, wananchi
wote wana jukumu la kuzilinda barabara na kuzitunza kwani ni muhimu katika
shughuli za maendeleo kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali na kushirikiana
kuwabaini wanaohujumu miunndombinu hiyo ili wafikishwe kwenye vyombo vya
sheria.
Aidha,Mkuu wa Mkoa
amemtaka Wakala wa barabara wa Mkoa kuwaelimisha watumiaji wa barabara matumizi
ya alama mbalimbali za barabara na kufanyia matengenezo alama zilizoharibiwa.
Katika kikao hicho
wajumbe wameazimia Mkoa uandae Kamusi ya mtandao wa Barabara unaoonesha
barabara zote katika Mkoa wa Shinyanga wenye urefu wa Kilometa 5,126.22.
Vilevile mkoa
unatarajia kujenga barabara moja yenye manufaa kiuchumi inayounganisha Mkoa wa
Shinyanga na Mkoa wa Mwanza kupitia Halmashauri za Manispaa ya Shinyanga,Wilaya
ya Shinyanga na Halmashauri ya Mji Kahama na Halmashauri ya wilaya ya Msalala
ambapo upembuzi yakinifu umeshafanyika na itagharimu jumla ya Tshs.Bilioni 118.
Hoja nyingine muhimu
iliyojadiliwa na wajumbe wa kikao hicho ni uzito wa mizigo ambao hauendani na
uwezo wa barabara, ambapo wajumbe wametaka alama zinazoonesha uwezo wa barabara
ili kudhibiti uzito wa mizigo inayozidi na inayoletea uharibifu wa barabara.
Meneja wa Wakala wa
barabara Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Philipo Manenuka amesema sheria ya kuweka
alama za kuonesha uzito wa barabara inatamka kuwa ni mamlaka yenyewe ya
serikali za mitaa ndiyo inaamua.
Na Magdalena Nkulu
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shinyanga.
0 comments:
Post a Comment