Home » » Chadema wamtimua Shibuda kikaoni

Chadema wamtimua Shibuda kikaoni


Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi (Chadema),John Shibuda
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi (Chadema), John  Shibuda amejikuta katika wakati mgumu, baada ya kuzuiwa asishiriki katika kikao cha viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki ya chama hicho kilichofanyika mjini Shinyanga.
 Hatua ya kuzuiwa kwa Mbunge huyo kushiriki katika kikao hicho ilitokana na hoja iliyotolewa na mjumbe kutoka Mwibara mkoani Mara, Ahmed Nkunda akidai hapaswi kushiriki baada ya kudai ni msaliti na amekuwa akikipongeza mara kwa mara Chama cha Mapinduzi (CCM).

 Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida wakati mbunge huyo akiamua kutoka nje kwa hiari yake mwenyewe alizuiwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe aliyekuwa akiongoza kikao hicho kwa madai mpaka kwanza wajumbe wote waafiki hoja hiyo.

Kutokana na hali hiyo Mbowe aliamua kuendesha zoezi la upigaji kura za ndiyo na hapana ili kuona ni wangapi waliokuwa wakiunga mkono hoja na wale wasioafiki, ambapo baada ya kuhesabiwa kwa kura za vidole wajumbe 90 waliunga mkono hoja huku 30 wakiipinga na hivyo kutakiwa atoke nje ya kikao.

 Hata hivyo mmoja wa wajumbe waliotaka mbunge huyo abaki ndani ya kikao alisema uhesabuji wa kura uliofanywa na Mbowe haukuwa sahihi kutokana na watu waliohesabiwa kuwa wa upande mmoja na kwamba hali hiyo ilisababisha wajumbe wengine pia waungane na Shibuda kutoka nje.

 Shibuda akizungumza na waandishi wa habari jana, alielezea kusikitishwa na kitendo kilichofanyika cha Mbowe  kuwalazimisha kumpigia kura wakati yeye mwenyewe alishaamua kutoka nje mapema ili kuepusha shari.

Shibuda alisema madai yanayotolewa kuwa yeye ni msaliti si ya kweli na kufafanua kuwa anachokifanya kila mara ni kuwatetea wapiga kura katika jimbo lake ili kuishinikiza serikali ya CCM iweze kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwamo kero za wafugaji na wakulima wa zao la pamba.

Alisema baadhi ya wanachama wa Chadema wakiwamo viongozi wakuu wa kitaifa walilaani kitendo chake cha kupanda katika jukwaa la CCM kule wilayani Meatu wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Taifa wa CCM, Abdulrahaman Kinana, lakini alisema alikwenda pale kwa lengo la kupeleka kilio cha wakulima wa pamba katika jimbo lake.

“Mimi siyo msaliti kwa maana nilichokifanya ni kutetea haki na maslahi ya wapiga kura wangu, wakulima na wafugaji, pale Meatu nilipanda katika jukwaa la CCM kumweleza Katibu Mkuu wa chama hicho matatizo ya wapiga kura wangu, maana yeye ndiye mwenye serikali iliyoko madarakani hivi sasa.”

“Ukweli ni kwamba hakuna njia ya mkato ya wananchi kutatuliwa kero zao bila ya kupitia chama tawala, wakulima wa pamba na wafugaji wanahitaji tiba badala ya maneno matupu ya ukuwadi na uwakala wa kuwapumbaza kisiasa, sasa utatuzi wa matatizo yao ni serikali ya CCM iliyoko madarakani, sisi wapinzani kazi yetu ni kushinikiza utekelezaji wake,” alieleza Shibuda.

Katika hatua nyingine mbunge huyo amewatahadharisha wanasiasa wanaoendekeza sera za makundi iwe ndani ya vyama vya upinzani ama chama tawala badala ya kuwatumikia Watanzania, na kwamba yeye daima atakuwa ni msemakweli na anapanga kwenda kwa wananchi wake kuwaeleza ukweli wote kwa nini anaonekana ni msaliti ndani ya chama chake.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa