WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowossa na Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza, Khamis Mgeja, wamechangisha sh milioni
9.2 katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo Kidogo cha Polisi cha
Kata ya Didia, wilayani Shinyanga, mkoani hapa.
Katika harambee hiyo, Mgeja na marafiki zake walichangia sh
5,830,000, huku Lowassa akichangia mifuko 100 ya saruji pamoja na fedha
taslimu sh 300,000.
Kwa upande wao wakazi wa kata hiyo walichanga sh 3,559,500, hivyo
kuvuka lengo la kukusanya sh 8,300,000 zilizokusudiwa kwa ajili ya
ujenzi wa kituo hicho cha polisi.
Akizungumza katika harambee hiyo, Mgeja mbali ya kuwapongeza wakazi
wa kata hiyo kwa uamuzi wao wa busara, pia aliziagiza halmashauri za
wilaya, miji, manispaa na majiji nchini kuweka utaratibu wa kutenga
bajeti katika halmashauri zao kwa ajili ya shughuli za ulinzi na
usalama.
Mgeja alisema suala la ulinzi na usalama ni sera ya CCM na
limeainishwa wazi ndani ya Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015,
hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa.
“Wakumbuke kuwa suala la ulinzi na usalama wa mali za wananchi wao
limo mikononi mwao, wananchi hawa wanapaswa kuhakikishiwa ulinzi katika
maeneo yao pale wanapotekeleza shughuli zao mbalimbali za maendeleo
ikiwamo shughuli za kibiashara na uwekezaji kwa wawekezaji kutoka nje
ama ndani ya nchi,” alieleza Mgeja.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
0 comments:
Post a Comment