Home »
» Makada CCM wakerwa kuitwa makarai
Makada CCM wakerwa kuitwa makarai
|
|
WAJUMBE wa Halmashuari za CCM wa kata mbalimbali wilayani
Kahama wamedai sababu ya wao kuitwa makarai na wanasiasa wa upinzani
inasababishwa na viongozi wa chama chao kuwatelekeza mara baada ya
uchaguzi.
Makada hao ambao walionyesha kukerwa na kauli za wanasiasa hasa wa
upinzani za kuwaita makarai ambayo hutumika wakati wa ujenzi na kazi
ikiisha husahaulika, walitoa kauli hiyo mbele ya Katibu wa Siasa na
Uchumi wa CCM Wilaya ya Kahama, Isaya Bukakiye kutokana na kukithiri kwa
umaskini miongoni mwao.
Walidai kuitwa makarai ni kauli inayowadhalilisha hasa kutokana na
wengi wao kuwa maskini baada ya uchaguzi kumalizika huku wakiwa
wamejitoa kwa nguvu kubwa kuhakikisha viongozi wa chama chao wameshinda,
ambao baadaye hujineemesha wenyewe na kuwaacha wapiga kura.
Katika madai hayo, waliiomba CCM kuwajengea uwezo kwa kuimarisha
vikundi vyao ujasiriamali, jambo ambalo litawasaidia kujikwamua
kiuchumi na kuwazidishia ari ya kukipigania chama chao kuliko ilivyo
sasa.
Akizungumzia madai hayo, Katibu wa Siasa na Uchumi wa CCM Wilaya ya
Kahama, Bukakiye, alisema ili kujikwamua na umaskini lazima waimarishe
vikundi na kwa kuanzia alitoa sh 500,000 kwa kikundi cha kina mama cha
Isanga.
Aidha, katika Kijiji cha Itumbo aliwachangia mifuko ya saruji 100 kwa
ajili ya ujenzi wa zahanati ambapo kikundi cha vijana wajasiriamali wa
Ukune aliwachangia kuku ishirini wa mayai pamoja na shilingi laki
tatu.
Ili kuondokana na kuitwa makarai aliwashauri Wana CCM kufanya kazi
kwa bidii kuliko kusubiri msimu wa uchaguzi kuomba fedha kutoka kwa
wagombea, hali ambayo alidai haiwezi kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment