Mbunge wa Maswa
Magharibi, mkoani Simiyu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Bw. John Shibuda, amewaomba viongozi wa vyama vya siasa
nchini
kuacha ubinafsi badala yake wajali masilahi ya umma.
Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi Mjini
Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari siku chache baada ya
kufukuzwa kwenye kikao cha viongozi wa CHADEMA,Kanda ya Ziwa Mashariki,
akidaiwa kukisaliti chama.
Alisema tabia ya baadhi ya viongozi wakuu wa
vyama vya siasa kutanguliza mbele masilahi binafsi, imechangia kutokea
mgawanyiko ndani ya vyama hivyo na kuua demokrasia.
Aliongeza kuwa, baadhi ya viongozi wa
upinzani wamekuwa wakifanya kila mbinu kwa lengo la kuwagawa wanachama
ili kujijengea mazingira ya kuendelea kukaa madarakani hata kama sehemu
kubwa ya wanachama imewachoka.
"Viongozi wanachangia migogoro ndani ya
vyama vya siasa kwa mfano, hivi sasa ndani ya CHADEMA lipo
tatizo...viongozi wetu wanafanya kila juhudi kujijengea mazingira ya
kubaki madarakani miaka yote.
"Suala hili halipo CHADEMA peke yake, karibu
vyama vyotevya siasa hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambako
makundi yamemeshamiri sana, leo hii viongozi wanasahau jukumu lao la
kuwatumikia wananchi badala yake wanlumbana wao kwa wao," alisema.
Aliwapa pole viongozi wa kisiasa ambao wanaoendekeza sera ya makundi ndani ya vyama vyao, kutunga hoja chafu ili wanachama
wawachukie baadhi ya watu ndani ya chama na kuonekana wasaliti.
"Niwathibitishie wazi kuwa, daima paka na
panya hawawezi kukaa chumba kimoja na haki ya dhuluma haviwezi kukaa
pamoja, lazima viongozi tuwajibike kwa wananchi," alisema Bw. Shibuda.
Bw. Shibuda alisema baada ya kufukuzwa ndani
ya kikao cha CHADEMA, dhamira yake ni kwenda kuwaeleza wananchi jimboni
kwake ukweli wote ili waelewe kwanini anaonekana msaliti katika chama
hicho na daiwa ataendelea kusimamia ukweli.
"Daima nitasimamia ukweli, nitawaeleza wananchi wangu ukweli wote na wao ndio wataamua kama utetezi ninaoufanya kwa ajili
ya wakulima na wafugaji jimboni ni usaliti, nitagombana na yeyote anayetaka kuharibu masilahi ya umma," alisema.
chanzo;majira
0 comments:
Post a Comment