Home » » Polisi waua watatu mgodi wa Bulyanhulu

Polisi waua watatu mgodi wa Bulyanhulu

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala
 
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika kijiji cha Namba Tisa kata ya Bulyanhulu Tarafa ya Msalala wilayani Kahama mkoani hapa wakati wakiwa katika harakati za kufanya uhalifu kwenye mgodi wa dhahabu wa  Bulyanhulu.
Watu hao ambao hawajafahamika majina yao, wana umri wa kati ya miaka 25 na 30.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala (pichani), alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati watuhumiwa hao wakiwa katika harakati za kuvamia mgodi wa dhahabu Bulyanhulu.

Kamanda Mangala alisema wakati watu hao wakiwa katika harakati za kufanya uhalifu huo, walianza kurushiana risasi na polisi.

Hata hivyo, alisema watu hao walizidiwa nguvu na polisi na kusababisha vifo vyao.

Kamanda Mangala alifafanua kuwa baada ya kuwaua watuhumiwa hao, polisi walikamata silaha za kivita yakiwamo mabomu matatu ya kurushwa kwa mkono na bunduki mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG) zenye namba 1972px7482 na ya pili yenye namba UC-17751998 pamoja na risasi 94 zikiwa kwenye magazine nne.

Alisema watu hao wanadaiwa walipanga kupora mali katika mgodi huo lakini walikwama baada ya polisi kupewa taarifa kutoka kwa wanakijiji na kufika eneo hilo.

Kamanda Mangala aliongeza kuwa baada ya kufika eneo la tukio, watuhumiwa hao walianza kurushiana risasi na polisi lakini walizidiwa nguvu na kuuawa wote.

Aidha, alisema miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ikisubiri kutambuliwa na ndugu zao.

Alitoa wito kwa wananchi mkoani humu kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapohisi kutokea uhalifu ili kudhibiti matukio hayo mapema.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa