IMEELEZWA sababu ya kutishia kuibuka kwa ukame katika maeneo
yaliyokuwa tegemeo kwa kilimo wilayani Kahama, ni udhaifu wa kusimamia
sheria ya misitu pamoja na kilimo cha zao la tumbaku.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alibainisha hayo juzi wakati
wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika Halmashauri ya Ushetu
iliyofanyika kijiji cha Kangeme, Kata ya Ulowa.
Alisema udhaifu huo unatokana na wanaohusika kufanya kazi kwa mazoea
kiasi cha kushindwa kusimamia sheria huku wanaohusika na zao la tumbaku
nao wakishindwa kuwajibika ipasavyo katika kutoa elimu juu ya umuhimu
wa upandaji miti.
Mpesya alisema ni wajibu wa Halmashauri ya Ushetu kutambua athari
inayoweza kusababisha kuibuka kwa ukame kwa kuwahamasisha wakulima wa
zao hilo kuona umuhimu wa kupanda miti huku ikisimamia sheria kwa
atakayeharibu miche na miti itakayopandwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema uoto wa asili uliokuwepo katika miaka
ishirini iliyopita katika eneo la Halmashauri ya Ushetu imeathiriwa kwa
kiwango kikubwa na wakulima wa zao la tumbaku kwa kukata magogo ya
miti ya kukaushia zao hilo.
“Leo hii tunajivunia kula matunda yaliyopandwa na wazee wetu miaka
mia moja iliyopita… sisi tunakata miti pasipo kuwaandalia kizazi
kijacho urithi wa miti,” alisema Mpesya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Isabela Chilumba,
alisema zao la tumbaku ni muhimu kwa ustawi wa halmashauri hiyo, na
kilimo hicho kuwa endelevu kunategemea uwepo wa misitu ya kutosha, na
kwa kutambua hilo ndiyo maana wameanzisha kampeni hiyo itakayofanyika
kila mwaka maeneo yote ya Ushetu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment