Tangu tuanze kuichambua mada hii ya maradhi ya saratani ya
ngozi, tumeangazia mambo mbalimbali ikiwamo saratani ni nini, aina za
saratani, makundi ya watu yanayoathiriwa zaidi na saratani hii ya ngozi.
Saratani si tu kwamba ni ugonjwa hatari lakini
pia ni ugonjwa unaompa mwanadamu mateso makali. Haijalishi ni saratani
ya ngozi, ya tumbo au ya kizazi.
Vilevile ni ugonjwa ambao matibabu yake
yanahitaji gharama kubwa mno. Inasemekana kuwa mgonjwa mmoja wa saratani
ambaye saratani yake imechelewa kugundulika, huhitaji kiasi cha Sh
300,000 kwa ajili ya matibabu.
Tatizo jingine ni kuwa kutokana na elimu duni,
Watanzania wengi hushindwa kupima saratani na kuigundua mapema hivyo
hugundulika katika hatua za mwisho.
Leo tutachambua kwa undani ukubwa wa tatizo hili kwa kuangalia ni ugonjwa wa hatari kiasi gani.
Melanoma ni saratani ya hatari sana kwa maisha ya
mwanadamu. Ni mara chache sana saratani hii hushambulia watu lakini
inapotokea mtu akapata saratani hii basi maisha yake yanakuwa hatarini
sana.
Saratani hii si rahisi kuigundua ukilinganisha na saratani nyingine za ngozi nilizokwisha taja hapo juu.
Siyo tu kwamba saratani hii ni ngumu kidogo kuitambua lakini pia husambaa haraka zaidi kuliko saratani nyingine za ngozi.
Melanoma huweza kusambaa na kushambulia viungo
vingine zaidi ya ngozi kama mifupa na ubongo. Inapofikia hatua hii
saratani hii inakuwa ngumu sana kutibika.
Dalili za Melanoma
Dalili ya kwanza kabisa ambayo inabidi kila mtu
afahamu ni kubadilika kwa ukubwa, rangi au ule muundo wa alama ya ngozi
ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu au umezaliwa nayo. Alama hii ni ile
ambayo ina rangi nyeusi zaidi ukilinganisha na maeneo mengine ya ngozi.
Mabadiliko haya si lazima yawe yanatokea haraka
haraka yanaweza kuwa yanatokea taratibu katika kipindi cha miezi lakini
cha muhimu ni kuwa unaona kabisa mabadiliko kwenye alama hiyo ya ngozi.
Ni muhimu sana kutambua mabadiliko haya. Mabadiliko mengine ni kama yafuatayo
Pamoja na mabadiliko niliyokwisha taja hapo juu alama hii inaweza kuwa inavimba,
kingo zake zinapoteza mzingo wake wa kawaida,
alama inakua zaidi kwa eneo (mfano kutoka mzingo wa 4 mm inakuwa kubwa na kuzidi 6 mm).
Alama inaweza kuanza kuwasha kama mgonjwa atachelewa kugundua tatizo basi dalili zifuatazo huonekana:
Alama ya kwenye ngozi kupasuka na kufanya kidonda
Alama kutoa damu
Kuwa na maumivu kwenye alama
Kama matibabu hayatofanyika basi saratani hii husambaa na dalili zifuatazo huweza kuonekana :
Tezi za mwili kuvimba (hususan zilizo kwenye makwapa na kwenye nyonga)
Uvimbe kwenye ngozi
Kupoteza uzito kwa kasi bila kujua sababu
Kikohozi kisichoisha
Kupoteza fahamu (Kifafa)
Kichwa kuuma
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment