Magonjwa ya moyo yameshika kasi hapa nchini kiasi cha kutishia uhai wa watu wengi.
Ripoti ya iliyotolewa na Taasisi ya Afya ya
Ifakara hivi karibuni inaeleza kuwa hospitali na zahanati nyingi hazina
vipimo vya moyo. Hali hii inatishia usalama wa afya za watu ambao
wanakwenda kwenye zahanati hizi lakini hawapati tiba sahihi na badala
yake wanaambulia kupimwa malaria tu.
Hata hivyo maradhi haya kwa asilimia 8o
yanazuilika kama hatua za mapema zitachukuliwa. Ndiyo maana upo usemi
usemao, kinga ni bora kuliko tiba hivyo ni vema kuchukua hatua mapema
kuliko kusubiri tatizo likukumbe.
Pale unapoona dalili zisizo za kawaida fika
haraka katika huduma za afya kwa ushauri, ikumbukwe kuwa gharama za
kutibu magonjwa haya huwa ni kubwa ukilinganisha na magonjwa mengine pia
muda wa kukaa hospitalini huwa ni mrefu.
Tatizo la moyo linaweza kuanza na kupotea kwa muda
mfupi lakini usipolitatua mapema huenda likawa sugu hivyo kuhitaji
matibabu ya kina na kukugharimu maishani.
Leo tunaendelea makala yetu ya moyo kushindwa kufanya kazi, nitaeleza kifupi matibabu, uchunguzi na namna yakujikinga.
Matibabu na uchunguzi
Ingawa pia yapo mambo mengi ya kuchunguza yaani maabara na picha nitagusia yale ya yanayohusu picha maalum za mwili.
Uchunguzi wa msingi unahusisha picha ya xray ya kifua kuona ukubwa wa moyo na uwepo wa maji katika mapafu.
Kipimo cha ‘echocardiogram-kipimo hiki huchunguza
sehemu za moyo kama vile chemba, vyumba, valvu, mishipa na mfumo wa
vimishipa vya fahamu katika moyo.
Kipimo cha electrocardiography-ECG-kuangalia
shinikizo la damu, mapigo ya misuli ya moyo, kuoza kwa misuli ya moyo na
hali ya kiumeme katika moyo.
Baada ya daktari wako kukufahamisha kutokana na dalili ulizonazo ndipo atafanya uamuzi ama upewe dawa au usipewe dawa.
Kupumzika muda mrefu ili usiuchoshe moyo wako
wenye tatizo lakini pia mgonjwa anatakiwa alale katika mkao maalum
utakaosaidia apumue vizuri yaani mito zaidi ya mwili huwekwa nyumba ya
mgongo na kichwa. Kama kuna kitanda maalum robo ya kitanda huinuliwa juu
kidogo.
Kutotumia chumvi na kunywa maji kipindi cha
ugonjwa. Mambo mengine ya kuzingatia ni kula mlo usio na mafuta mengi ya
wanyama, kula mboga na matunda zaidi katika kila mlo na vyakula
visivyokobolewa.
Matibabu ya dawa huwa ni maisha yako yote, kama
vile unavyomwona punda akivuta toroli kubwa lenye mzigo mzito kwa tabu,
ili mnyama huyu aweze kuvuta toroli kwa urahisi inabidi kupunguza mzigo
na kuuweka pembeni ili aweze kusonga mbele.
Mfano huo ndivyo dawa za moyo zinavyofanya kazi
ili kuurudisha moyo katika hali ya kawaida na kufanya kazi ya kusukuma
damu. Katika huduma za afya wataalam wa moyo watakuelimisha zaidi juu ya
madhara ya dawa na ugonjwa kwa mfano ushauri nasaha wa tatizo
linalowapata wagonjwa hawa huwa na upungufu wa nguvu za kiume kwa
kipindi cha ugonjwa lakini baada ya kupata nafuu mtu hurudi katika hali
yake.
Dawa ni kama vile za kupunguza mrundikano wa maji
mwilini, kuifanya misuli ya mwili ikunjuke zaidi na kusukuma damu, dawa
za kutanua mishipa ya damu na mwisho ni kutibu tatizo lililosababisha
moyo kushindwa kufanya kazi.
Yapo baadhi ya magonjwa ya moyo yanayosababisha moyo kushindwa kufanya kazi ambayo kwa kawaida huwa hayaponi.
Hivyo dawa nyingi ni zile zakusaidia moyo ufanye
kazi vizuri, na dawa hizi unapaswa kutumia kufuatana na maelekezo ya
daktari kwani endapo utazidisha kipimo zina madhara na pengine
kusababisha moyo kusimama na hatimaye kifo.
Namna ya kujikinga na tatizo hili kiujumla
Fika mapema katika huduma za afya pale unapoona
dalili, jenga utamaduni wa kupima mapigo yako ya moyo, sukari ya mwili
na kiwango cha lehemu mwilini (cholestrol) hii inasaidia kujua mwenendo
wa afya yako.
Lehemu ni mafuta mabaya yanayosababisha kuharibika mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo.
Kufanya mazoezi mara kwa mara na mapema kabla ya kupata matatizo ya kiafya ni nzuri kwa afya yako
Mazoezi yanaufanya mwili utumie mafuta ya ziada yaliyorundikana
mwilini na pia kuufanya mwili kuwa na mzunguko mzuri wa damu, angalau
mazoezi ya kutembea kwa siku kwa dakika 15-30 yanatosha.
Epuka hasira, shinikizo la kiakili na sonona.Epuka
matumizi ya pombe kupita kiasi na tumbaku kwani vitu hivi vina madhara
katika moyo na mishipa ya damu.
Ugonjwa wa moyo huweza kumpata mtu yeyote bila
kujali umri, na katika siku za karibuni mtindo wa maisha umewafanya watu
wengi kupata maradhi haya kutokana na ulaji holela wa mlo usiozingatia
afya na kuacha kufanya mazoezi.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment