Home » » AHOJIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI VIONGOZI CHADEMA

AHOJIWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI VIONGOZI CHADEMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katibu Mkuu wa Chadema,Dk. Willibrod Slaa.
 
Jeshi la Polisi mkoani hapa, linamhoji aliyekuwa Diwani wa Kata ya Masekelo ya Manispaa ya Shinyanga, Zacharia Mfuko kuhusiana na  tuhuma alizotoa za kuwapo kwa njama za mauaji ya viongozi kadhaa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kurejea tena Chadema, alianza kuhojiwa jana na Mkuu wa Upelelezi Mkoa  (RCO) wa Shinyanga, Mussa Athumani kuanzia  saa 6:00 mchana kuhusiana na kuibua tuhuma hizo pamoja na mwenzake, Sebastian Peter.

Ilidaiwa kuwa mbele ya hadhara, diwani huyo alisema kuna njama za kuwaua viongozi wa Chadema, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa na Mwanasheria wao mkuu, Tundu Lisu, kwa kutungua ndege yao wakati walipokuwa wakiwasili kwenye mkutano wa hadhara mjini Shinyanga.

Kufuatia tuhuma hizo, ndipo jeshi hilo lilipoanza kufanya upelelezi kwa  kufuatilia mtandao unaodaiwa kupanga mauaji hayo, ikiwamo kwa kumhoji diwani huyo na mwenzake (Peter) ambaye hakuwapo kituoni hapo jana baada ya kuelezwa kuwa ana udhuru.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Shinyanga,  Hassan Baruti, alisema  Peter aliyekuwa Diwani wa  Kata ya Ngokolo, yupo njiani akitokea  Kigoma na hivyo atawasili usiku na kuhojiwa leo.

WAFUASI CHADEMA
Wakati mtuhumiwa huyo akihojiwa,  wafuasi wa Chadema walikusanyika nje ya kituo cha polisi wakisubiri atolewe huku wakidai hawatakubali awekwe rumande.

Hadi NIPASHE linaondoka kituoni hapo, mtuhumiwa huyo alikuwa akiendelea kuhojiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Justus Kamugisha hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

Jumamosi ya wiki iliyopita, ‘madiwani’ walioasi Chadema na kurejea, walifanya mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho na kudai kuwa walirubuniwa na makada watano wa CCM kuhama Chadema ili wawatumie kuwaua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama hicho, John Mnyika.

‘Madiwani’ hao, ni Sebastian Mzuka wa Kata ya Ngokolo na Zacharia Martin wa Kata ya Masekelo wote kutoka Shinganya mjini, ambao waliwataja makada hao kuwa ni Naibu wa Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Wengine ni Steven Masele, ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, na Habibu Mchange (aliyefukuzwa Chadema).

Madiwani hao walisema mauaji hayo yalipangwa kutekelezwa kwa kiasi cha Sh. milioni 180.Diwani Mzuka alisema walifika kwenye ofisi hizo ili kueleza kinachoendelea kudhoofisha chama na kuomba toba baada ya kuhama.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Shinyanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa