Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WITO umetolewa kwa watanzania kuacha kuzibeza shule za sekondari za
kata badala yake waziamini na kuziunga mkono hasa kwa kuwa kipindi hiki
ambapo shule hizo zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Mkuu wa shule ya sekondari Mwendakulima wilayani Kahama Shinyanga,
Diana Kuboja alisema hayo alipowapongeza wanafunzi 15 kati ya 23
waliofaulu kidato cha sita kwa daraja la kwanza shuleni hapo.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya African Barrick Gold
Mine (ABG) kupitia mgodi wake wa Buzwagi, Diana alisema matokeo ya mwaka
huu kidato cha sita wanafunzi wote 23 wa shule yake wamefaulu kati yao
nane walipata daraja la pili na waliobaki walipata daraja la kwanza.
“Mwendakulima imekua ya kwanza kimkoa na kikanda… kitaifa kwa shule
zenye wanafunzi 180 imekuwa ya tisa, hivyo jamii inapaswa kuheshimu
matokeo hayo,” alisema mkuu huyo wa shule.
Alisema serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa
kuleta walimu wenye taaluma hivyo ni budi jamii nayo ikatoa msaada wa
kuboresha mazingira ya miundombinu na majengo kwa kushirikiana na
wafadhili hatua itakayozidisha hamasa ya kufanya vema kwa sekodari za
kata.
“Si sahihi shule hizi kuziita yeboyebo na kauli hiyo ni changamoto
kwetu kuuhakikishia umma kuwa tunaweza… jamii itambue ubora wa shule
zetu,” alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka ABG na Mkurugenzi wa Bodi ya
Ufadhili wa ‘Can Educate’ ya jijini London Uingereza, Katrina White
alisema kampuni yake imeongeza Dola 5,000 za Marekani kwenye ufadhili
katika huduma za jamii kwa maeneo jirani na migodi.
Meneja Mkuu wa mgodi wa Buzwagi, Philbert Rweyemamu ameitaka jamii
kuwa mstari wa mbele katika suala zima la maendeleo kuliko kutegemea
mgodi huku akibainisha kwamba mgodi wake umefadhili wanafunzi 400 wa
shule za msingi katika kata hiyo wakati wanafunzi 200 wa sekondari
wamepata ufadhili huo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment