CHAMA Kikuu cha Ushirika wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga (KACU),
kimepata viongozi wapya wa Bodi huku mjumbe mmoja akitaka kujivua
madaraka hayo ya ujumbe baada ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha
kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya ushirika huo.
Uchaguzi huo wa kuwapata wajumbe wa bodi ya Ushirika huo unaojumuisha
vyama vya Msingi vya wakulima kutoka Wilaya za Kahama na Bukombe,
ulifanyika juzi katika ukumbi wa Halmashauri ya Ushetu.
Dosari katika uchaguzi huo, ilijitokeza baada ya aliyekuwa Mwenyekiti
wa KACU kwa miaka mitatu, Said Tangawizi, kushindwa kutetea nafasi
hiyo na kuomba kujiengua ili kumpa fursa Mwenyekiti mpya kufanya kazi
kwa kujiamini.
Tangawizi aliyepata ujumbe kupitia Wilaya ya Bukombe, aliingia katika
kinyang’anyiro cha kutetea nafasi yake ya Uenyekiti lakini alishindwa
kwa kura tatu na Makamu Mwenyekiti wake, Emmanuel Cherahani, ndipo
aliposimama wakati wajumbe wakiendelea na zoezi la upigaji kura nafasi
nyingine na kudai anajiuzuru ujumbe wa Bodi.
“Nakiri kushindwa na ninampongeza aliyekuwa Makamu wangu kunibwaga,
na ili kumpa nafasi ya kujitanua katika utekelezaji wa majukumu yake,
ni vyema nikajiuzuru ujumbe nilionao ili isije tokea akashindwa kufanya
kazi kwa ufanisi kwa ajili yangu,” alisema Tangawizi.
Hata hivyo, Mwakilishi wa Mrajis kutoka Dodoma, Moshi Chogero,
alipinga uamuzi huo kwa maelezo unakwenda kinyume cha kanuni na
taratibu za chaguzi za vyama vya Ushirika nchini.
Aidha, Chogero aliwaasa viongozi waliochaguliwa kuwa waadilifu kwa
mali za Ushirika, kwa kuhakikisha wanaepuka kuuingiza Ushirika katika
hasara na kuondoa hasara zilizokwishapatikana sambamba na kuwachukulia
hatua ikiwemo kuwafilisi mali zao waliokwishafanya ufisadi ndani ya
Ushirika.
Katika uchaguzi huo, wajumbe waliochaguliwa kutoka Wilaya za Mbogwe
na Bukombe ni Yilagela Chabili (Makamu Mwenyekiti), huku wajumbe ni
Wales Bundala na Said Tangawizi wakati kutoka Ushetu na Kahama ni
Seslia Maligo, Paul Lugomya na Geofrey Mondo.
Wajumbe waliochaguliwa kuuwakilisha ushirika huo katika vikao vya
Apex ni pamoja na Mwenyekiti wa Ushirika huo, Cherahani na Wales
Bundala huku kutoka nje ya Bodi ni Rashid Ally Hamis.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment